Amosi

Amosi

1

1 Maneno ya Amosi, aliyekuwa mmoja wa wachungaji wa Tekoa; maono aliyoyaona katika habari za Israeli, siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli, miaka miwili kabla ya tetemeko la nchi.

2 Naye alisema, Bwana atanguruma toka Sayuni, Atatoa sauti yake toka Yerusalemu; Na malisho ya wachungaji yataomboleza, Na kilele cha Karmeli kitanyauka.

3 Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Dameski, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameipura Gileadi kwa vyombo vya kupuria vya chuma;

4 Lakini nitapeleka moto uingie katika nyumba ya Hazaeli, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi.

5 Nami nitalivunja komeo la Dameski, na kuwakatilia mbali wenyeji wa bondeni mwa Aveni, na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Beth-Adini; na watu wa Shamu watakwenda hali ya kufungwa hata Kiri, asema Bwana.

6 Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Gaza, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu waliichukua katika hali ya kufungwa kabila nzima, wawatie katika mikono ya Edomu;

7 Lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Gaza, nao utayateketeza majumba yake.

8 Nami nitamkatilia mbali mwenyeji katika Ashdodi; na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Ashkeloni; nami nitaugeuza mkono wangu uwe juu ya Ekroni; na mabaki ya Wafilisti wataangamia, asema Bwana MUNGU.

9 Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Tiro, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameitia kabila nzima katika mikono ya Edomu, wala hawakulikumbuka agano la udugu;

10 Lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Tiro, nao utayateketeza majumba yake.

11 Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Edomu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga, akatupilia mbali huruma zake zote; hasira yake ikararua-rarua daima, akaishika ghadhabu yake milele;

12 Lakini nitapeleka moto juu ya Temani, nao utayateketeza majumba ya Bosra.

13 Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya wana wa Amoni, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewapasua wanawake wa Gileadi wenye mimba, ili wapate kuongeza mipaka yao;

14 Lakini nitawasha moto katika ukuta wa Raba, nao utayateketeza majumba yake; pamoja na kupiga kelele siku ya vita, pamoja na tufani katika siku ya chamchela;

15 Na mfalme wao atakwenda utumwani, yeye na wakuu wake wote pamoja, asema Bwana.

More in this category: « Obadia Yoeli »

Login

Register

You need to enable user registration from User Manager/Options in the backend of Joomla before this module will activate.