1 Mambo ya Nyakati - Sura ya 12

1 Mambo ya Nyakati - Sura ya 12

1Basi hawa ndio wale waliomjia Daudi huko Siklagi, alipokuwa akijificha kwa ajili ya Sauli, mwana wa Kishi; nao walikuwamo miongoni mwa wale mashujaa, waliomsaidia vitani.

2Walikuwa wenye kupinda upinde, nao walikuwa hodari wa kutumia mkono wa kuume na wa kushoto, kwa kutupa mawe ya teo, na kwa kupiga mishale ya upinde; walikuwa wa nduguze Sauli, wa Benyamini.

3Mkubwa wao alikuwa Ahiezeri, kisha Yoashi, wana wa Shemaa Mgibeathi; na Yezieli, na Peleti, wana wa Azmawethi; na Beraka, na Yehu Mwanathothi;

4na Ishmaya Mgibeoni, shujaa wa wale thelathini, naye alikuwa juu ya wale thelathini; na Yeremia, na Yahazieli, na Yohana, na Yozabadi Mgederathi;

5Eluzai, na Yerimothi, na Bealia, na Shemaria, na Shefatia Mharufi;

6Elkana, na Ishia, na Azaleli, na Yoezeri, na Yashobeamu, Wakora;

7na Yoela, na Zebadia, wana wa Yerohamu, wa Gedori.

8Na wa Wagadi wakajitenga kumfuata Daudi ngomeni huko nyikani, waume mashujaa, watu waliozoea vita, walioweza kutumia ngao na mkuki; ambao nyuso zao zilikuwa kama nyuso za simba, nao walikuwa wepesi kama kulungu juu ya milima;

9Ezeri mkubwa wao, Obadia wa pili, Eliabu wa tatu;

10Mishmana wa nne, Yeremia wa tano;

11Atai wa sita, Elieli wa saba;

12Yohana wa nane, Elzabadi wa kenda;

13Yeremia wa kumi, Makbanai wa kumi na moja.

14Hao wa wana wa Gadi walikuwa maakida wa jeshi, yeye aliyekuwa mdogo amelingana na mia, na yeye aliyekuwa mkuu, na elfu.

15Hao ndio wale waliovuka Yordani katika mwezi wa kwanza, ulipofurika kingo zake zote; nao wakawakimbiza wote wa bondeni kuelekea mashariki na magharibi pia.

16Tena wakafika ngomeni kwa Daudi baadhi ya wana wa Benyamini na Yuda.

17Naye Daudi akatoka ili kuwalaki, akajibu, akawaambia, Kama mmenijia kwa amani ili kunisaidia, basi moyo wangu utaambatana nanyi; lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa adui zangu, kwa kuwa hamna udhalimu mikononi mwangu, Mungu wa baba zetu na alitazame neno hili, na kulikemea.

18Ndipo roho ikamjilia Abishai, mkuu wa wale thelathini, naye akasema, Sisi tu watu wako, Ee Daudi; Na wa upande wako, Ee mwana wa Yese; Amani, naam, amani iwe kwako, Na amani iwe kwao wakusaidiao; Maana akusaidiye ndiye Mungu wako. Ndipo Daudi akawakaribisha, akawaweka wawe maakida wa kile kikosi.

19Wa Manase pia wengine walimwangukia Daudi, alipokwenda pamoja na Wafilisti juu ya Sauli vitani, lakini hawakuwasaidia; kwani wale mabwana wa Wafilisti wakafanya shauri, wakamfukuza, wakisema, kwa hatari ya vichwa vyetu atamwangukia bwana wake Sauli.

20Naye alipokuwa akienda Siklagi, wakamwangukia hawa wa Manase, Adna, na Yozabadi, na Yediaeli, na Mikaeli, na Yozabadi, na Elihu, na Silethai, maakida wa maelfu waliokuwa wa Manase.

21Wakamsaidia Daudi juu ya kile kikosi kilichomshambulia; kwani walikuwa waume mashujaa wote, nao wakawa maakida jeshini.

22Maana siku kwa siku humjia Daudi watu wa kumsaidia, hata wakapata kuwa jeshi kubwa, kama jeshi la Mungu.

23Na hizi ni hesabu za vichwa vya watu wenye silaha za vita, waliokuja Hebroni kwa Daudi, ili kumgeuzia ufalme wa Sauli, sawasawa na neno la Bwana.

24Wana wa Yuda, waliochukua ngao na mkuki, walikuwa elfu sita na mia nane, wenye silaha za vita.

25Wa wana wa Simeoni, waume mashujaa wa vita, elfu saba na mia moja.

26Wa wana wa Lawi, elfu nne na mia sita.

27Na Yehoyada alikuwa kichwa cha mbari ya Haruni, na pamoja naye walikuwa elfu tatu na mia saba;

28tena Sadoki, kijana shujaa, na wa nyumba ya babaye, maakida ishirini na wawili.

29Na wa wana wa Benyamini nduguze Sauli, elfu tatu; kwani hata sasa walio wengi wao walikuwa wameuhifadhi uaminifu wao kwa nyumba ya Sauli.

30Na wa wana wa Efraimu, ishirini elfu na mia nane, waume mashujaa, watu wenye sifa katika mbari za baba zao.

31Na wa nusu kabila ya Manase, kumi na nane elfu, waliotajwa majina yao, ili waje kumtawaza Daudi awe mfalme.

32Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.

33Wa Zabuloni, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, wenye zana za vita za kila namna, hamsini elfu; askari wastadi wasiokuwa wenye moyo wa kusita-sita.

34Na wa Naftali, maakida elfu, na pamoja nao watu wenye ngao na mkuki thelathini na saba elfu.

35Na wa Wadani, watu hodari wa kupanga vita, ishirini na nane elfu na mia sita.

36Na wa Asheri, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, arobaini elfu.

37Tena, ng'ambo ya pili ya Yordani, wa Wareubeni, na wa Wagadi, na wa nusu kabila ya Manase, wenye zana za vita za kupigania za kila namna, mia na ishirini elfu.

38Hao wote, watu wa vita, askari wastadi, wakaja Hebroni wenye moyo mkamilifu, ili kumtawaza Daudi awe mfalme juu ya Israeli wote; tena wote waliosalia wa Israeli nao walikuwa na moyo mmoja kwamba wamtawaze Daudi.

39Nao walikuwako huko pamoja na Daudi siku tatu, wakila na kunywa; kwani ndugu zao walikuwa wamewaandalia tayari.

40Zaidi ya hayo, wale waliokuwa karibu nao, hata mpaka kwa Isakari, na Zabuloni, na Naftali, wakaleta chakula juu ya punda, na ngamia, na nyumbu, na ng'ombe, vyakula vya unga, mikate ya tini, na vichala vya zabibu kavu, na divai, na mafuta, na ng'ombe, na kondoo tele; kwa kuwa kulikuwa na furaha katika Israeli.