1 Mambo ya Nyakati - Sura ya 14

1 Mambo ya Nyakati - Sura ya 14

1Naye Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na waashi, na maseremala, ili wamjengee nyumba.

2Daudi akajua ya kwamba Bwana amemweka imara ili amiliki juu ya Israeli, kwa kuwa milki yake imeinuka kwa ajili ya watu wake Israeli.

3Tena Daudi akazidi kuoa wake huko Yerusalemu; akazidi Daudi kuzaa wana na binti.

4Na haya ndiyo majina ya watoto aliozaliwa huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani;

5na Ibhari, na Elishua, na Elpeleti;

6na Noga, na Nefegi, na Yafia;

7na Elishama, na Eliada, na Elifeleti.

8Na waliposikia hao Wafilisti ya kwamba Daudi ametiwa mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli wote, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akasikia, akatoka nje kupigana nao.

9Basi hao Wafilisti walikuwa wamekuja na kuteka nyara katika bonde la Warefai.

10Daudi akamwuliza Mungu, kusema, Je! Nipande juu ya Wafilisti! Utawatia mikononi mwangu? Naye Bwana akamwambia, Panda; kwa kuwa nitawatia mikononi mwako.

11Basi wakapanda mpaka Baal-perasimu, Daudi naye akawapiga huko; Daudi akasema, Bwana amewafurikia adui zangu kwa mkono wangu, kama mafuriko ya maji. Basi wakapaita mahali pale jina lake Baal-perasimu.

12Nao wakaiacha miungu yao huko; naye Daudi akaamuru, ikateketezwa kwa moto.

13Lakini hao Wafilisti wakateka nyara tena mara ya pili bondeni.

14Na Daudi akamwuliza Mungu tena; naye Mungu akamwambia, Hutapanda kuwafuata; uwageukie mbali, ukawajie huko kuielekea miforsadi.

15Kisha itakuwa utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo utakapokwenda nje vitani; kwa maana ndipo Mungu ametoka mbele yako, awapige jeshi la Wafilisti.

16Daudi akafanya kama vile Mungu alivyomwamuru; wakawapiga jeshi la Wafilisti toka Geba mpaka Gezeri.

17Sifa za Daudi zikafika nchi zote; naye Bwana akawaletea mataifa yote hofu yake.