1 Mambo ya Nyakati - Sura ya 17

1 Mambo ya Nyakati - Sura ya 17

1Ikawa, Daudi alipokuwa akikaa nyumbani mwake, Daudi akamwambia nabii Nathani, Angalia, mimi ninakaa katika nyumba ya mwerezi, bali sanduku la agano la Bwana linakaa chini ya mapazia.

2Naye Nathani akamwambia Daudi, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; kwa maana Mungu yu pamoja nawe.

3Ikawa usiku uo huo, neno la Mungu likamjia Nathani, kusema,

4Nenda, kamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Wewe hutanijengea nyumba ya kukaa;

5kwa maana sikukaa ndani ya nyumba tangu siku ile nilipowaleta Israeli huku hata leo; lakini hema kwa hema nimehamia, na maskani kwa maskani.

6Katika mahali mwote nilimokwenda na Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliowaagiza kuwalisha watu wangu, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mwerezi?

7Basi sasa ndivyo utakavyomwambia mtumishi wangu Daudi, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo ili uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli;

8nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina, kama jina la hao wakuu walioko duniani.

9Tena nitawaagizia watu wangu Israeli mahali, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena kama hapo kwanza,

10na tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi wawe juu ya watu wangu Israeli, nami nitawashinda adui zako wote. Pamoja na hayo nakuambia, ya kwamba Bwana atakujengea nyumba.

11Hata itakuwa, siku zako zitakapotimia, uende na babazo, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayekuwa wa wana wako; nami nitaufanya imara ufalme wake.

12Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakifanya imara kiti cha enzi cha ufalme wake milele.

13Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; wala sitamwondolea fadhili zangu, kama nilivyomwondolea yeye aliyekuwa kabla yako;

14ila nitamstarehesha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele; na kiti chake cha enzi kitathibitishwa milele.

15Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi.

16Ndipo akaingia Daudi mfalme, akaketi mbele za Bwana; akasema Mimi ni nani, Ee Bwana Mungu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa?

17Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Mungu; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja, nawe umeniangalia sawasawa na hali ya mtu mwenye cheo, Ee Bwana Mungu.

18Na Daudi akuambie nini tena zaidi kwa habari ya heshima aliyotendewa mtumwa wako? Kwa maana wewe umemjua mtumwa wako.

19Ee Bwana, kwa ajili ya mtumwa wako, na kwa moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote.

20Ee Bwana, hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu.

21Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake mwenyewe, ili wawe watu wake, na kujifanyia jina kwa njia ya mambo makuu, yenye kuogofya, kwa kufukuza mataifa mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri?

22Kwa maana watu wako Israeli ndio uliowafanya kuwa watu wako wa milele; nawe, Bwana, umekuwa Mungu wao.

23Basi sasa, Ee Bwana, neno lile ulilolinena katika habari za mtumwa wako, na katika habari za nyumba yake, na lifanywe imara milele, ukafanye kama ulivyosema.

24Jina lako na liwe imara, likatukuzwe milele, kusema, Bwana wa majeshi ndiye Mungu wa Israeli, naam, Mungu juu ya Israeli; na hiyo nyumba ya Daudi mtumwa wako imefanywa imara mbele zako.

25Kwa kuwa wewe, Ee Mungu wangu, umenifunulia mimi mtumwa wako ya kuwa utanijengea nyumba; kwa hiyo mimi mtumwa wako nimeona vema moyoni mwangu kuomba mbele yako.

26Na sasa, Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema;

27nawe sasa umekuwa radhi kuibarikia nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Bwana, umebarikia, nayo imebarikiwa milele.