1 Mambo ya Nyakati - Sura ya 18

1 Mambo ya Nyakati - Sura ya 18

1Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda, akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa Wafilisti.

2Akapiga Moabu; na hao Wamoabi wakawa watumwa wa Daudi wakaleta zawadi.

3Tena Daudi akampiga Hadadezeri, mfalme wa Soba, mpaka Hamathi, alipokwenda kujisimamishia mamlaka yake kwenye mto wa Frati.

4Daudi akampokonya magari elfu, na wapanda farasi saba elfu, na askari waendao kwa miguu ishirini elfu; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila wa magari mia akawaweka.

5Na Washami wa Dameski walipokuja wamsaidie Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akapiga katika hao Washami watu ishirini na mbili elfu.

6Ndipo Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski; nao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye Bwana akampa Daudi kushinda kila alikokwenda.

7Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumishi wa Hadadezeri akazileta Yerusalemu.

8Tena toka Tibhathi, na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno, aliyofanyizia Sulemani ile bahari ya shaba, na zile nguzo, na vile vyombo vya shaba.

9Hata aliposikia Tou, mfalme wa Hamathi, ya kuwa Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri, mfalme wa Soba,

10akampeleka mwanawe Hadoramu kwa mfalme Daudi, ili kumsalimia, na kumbarikia, kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou; naye akaleta vyombo vya dhahabu, na fedha, na shaba, vya namna zote.

11Hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa Bwana, pamoja na hiyo fedha na dhahabu, aliyoteka nyara kwa mataifa yote; kwa Edomu, na kwa Moabu, na kwa wana wa Amoni, na kwa Wafilisti, na kwa Amaleki.

12Tena Abishai, mwana wa Seruya, akawapiga wa Waedomi katika Bonde la Chumvi watu kumi na nane elfu.

13Akaweka ngome katika Edomu; na Waedomi wote wakawa watumwa wa Daudi. Naye Bwana akampa Daudi kushinda, kila alikokwenda.

14Basi Daudi akatawala juu ya Israeli wote; akawafanyia hukumu na haki watu wake wote.

15Na Yoabu mwana wa Seruya akawa juu ya jeshi; na Yehoshafati mwana wa Ahiludi mwenye kuandika tarehe.

16Na Sadoki mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki mwana wa Abiathari, walikuwa makuhani; na Shausha mwandishi;

17na Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi; na wana wa Daudi walikuwa wakuu kumzunguka mfalme.