Wakorinto - Sura ya 13

Wakorinto - Sura ya 13

1Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.

2Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.

3Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.

4Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;

5haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;

6haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;

7huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.

8Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.

9Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu;

10lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika.

11Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto.

12Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.

13Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.