Wakorinto - Sura ya 7

1Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke.
2Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.
3Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.
4Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.
5Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.
6Lakini nasema hayo, kwa kutoa idhini yangu, si kwa amri.
7Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi.
8Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo.
9Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.
10Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe;
11lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.
12Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache.
13Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.
14Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu.
15Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyo ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani.
16Kwa maana wajuaje, wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo?
17Lakini kama Bwana alivyomgawia kila mtu, kama Mungu alivyomwita kila mtu, na aenende vivyo hivyo. Ndivyo ninavyoagiza katika makanisa yote.
18Je! Mtu fulani ameitwa hali amekwisha kutahiriwa? Asijifanye kana kwamba hakutahiriwa. Mtu fulani ameitwa hali hajatahiriwa bado? Basi asitahiriwe.
19Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu.
20Kila mtu na akae katika hali ile ile ambayo alikuwa nayo alipoitwa.
21Je! Uliitwa u mtumwa? Usione ni vibaya lakini kama ukiweza kuwa na uhuru, afadhali kuutumia.
22Kwa maana yeye aliyeitwa katika Bwana hali ya utumwa, ni huru wa Bwana. Vivyo hivyo yeye naye aliyeitwa hali ya uhuru, ni mtumwa wa Kristo.
23Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa wanadamu.
24Ndugu zangu, kila mtu na akae mbele za Mungu katika hali iyo hiyo aliyoitwa nayo.
25Kwa habari za wanawali sina amri ya Bwana, lakini natoa shauri langu, mimi niliyejaliwa kwa rehema za Bwana kuwa mwaminifu.
26Basi, naona hili kuwa jema, kwa ajili ya shida iliyopo, kwamba ni vema mtu akae kama alivyo.
27Je! Umefungwa kwa mke? Usitake kufunguliwa. Umefunguliwa? Usitafute mke.
28Lakini, kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia; lakini watu kama hao watakuwa na dhiki katika mwili nami nataka kuwazuilia hayo.
29Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana;
30na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu.
31Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita.
32Lakini nataka msiwe na masumbufu. Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendezeje Bwana;
33bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe.
34Tena iko tofauti hii kati ya mke na mwanamwali. Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana, apate kuwa mtakatifu mwili na roho. Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mumewe.
35Nasema hayo niwafaidie, si kwamba niwategee tanzi, bali kwa ajili ya vile vipendezavyo, tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine.
36Lakini mtu awaye yote akiona ya kuwa hamtendei mwanamwali wake vipendezavyo, na ikiwa huyo amepita uzuri wa ujana wake, na ikiwapo haja, basi, afanye apendavyo, hatendi dhambi, na awaruhusu waoane.
37Lakini yeye aliyesimama kwa uthabiti wa moyo wake, hana sharti, lakini aweza kuyatawala mapenzi yake, tena amekusudia moyoni mwake kumlinda mwanamwali wake, atatenda vema.
38Basi, hivyo na amwozaye mwanamwali wake afanya vema; na yeye asiyemwoza atazidi kufanya vema.
39Mwanamke hufungwa maadamu mumewe yu hai, lakini ikiwa mumewe amefariki, yu huru kuolewa na mtu ye yote amtakaye; katika Bwana tu.
40Lakini heri yeye zaidi akikaa kama alivyo; ndivyo nionavyo mimi, nami nadhani ya kuwa mimi nami nina Roho wa Mungu.