Wakorinto - Sura ya 8

Wakorinto - Sura ya 8

1Na kwa habari ya vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga.

2Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.

3Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo amejulikana naye.

4Basi kwa habari ya kuvila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na ya kuwa hakuna Mungu ila mmoja tu.

5Kwa maana ijapokuwa wako waitwao miungu, ama mbinguni ama duniani, kama vile walivyoko miungu mingi na mabwana wengi;

6lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa yeye huyo.

7Bali ujuzi huu haumo ndani ya watu wote; ila wengine kwa kuizoelea ile sanamu hata sasa hula kana kwamba ni kitu kilichotolewa sadaka kwa sanamu; na dhamiri zao, kwa kuwa dhaifu, hunajisika.

8Lakini chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu; maana, tusipokula hatupunguziwi kitu, wala tukila, hatuongezewi kitu.

9Lakini angalieni huu uwezo wenu usije ukawakwaza wale walio dhaifu.

10Kwa maana, mtu akikuona wewe uliye na ujuzi, umeketi chakulani ndani ya hekalu la sanamu, je! Dhamiri yake mtu huyo, kwa kuwa yu dhaifu, haitathibitika hata yeye naye ale vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu?

11Na yule aliye dhaifu aangamizwa kwa ujuzi wako, naye ni ndugu ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.

12Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhamiri iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo.

13Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu.