1 Yohana - Sura ya 2

1 Yohana - Sura ya 2

1Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,

2naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.

3Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake.

4Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.

5Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake.

6Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.

7Wapenzi, siwaandikii amri mpya, ila amri ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Na hiyo amri ya zamani ni neno lile mlilolisikia.

8Tena nawaandikia amri mpya, neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu; kwa kuwa giza linapita na ile nuru ya kweli imekwisha kung'aa.

9Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.

10Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.

11Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.

12Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu, kwa ajili ya jina lake.

13Nawaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Nimewaandikia ninyi, watoto, kwa sababu mmemjua Baba.

14Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu.

15Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.

16Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.

17Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.

18Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho.

19Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu.

20Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote.

21Sikuwaandikia ninyi kwa sababu hamwijui iliyo kweli, bali kwa sababu mwaijua, tena kwamba hapana uongo wo wote utokao katika hiyo kweli.

22Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana.

23Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia.

24Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya Baba.

25Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele.

26Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza.

27Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.

28Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake.

29Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye.