1 Wafalme - Sura ya 18

1 Wafalme - Sura ya 18

1Ikawa baada ya siku nyingi, neno la Bwana likamjia Eliya, katika mwaka wa tatu, kusema, Enenda, ukajionyeshe kwa Ahabu; nami nitaleta mvua juu ya nchi.

2Basi Eliya akaenda ili ajionyeshe kwa Ahabu. Na njaa ilikuwa nzito katika Samaria.

3Ahabu akamwita Obadia, aliyekuwa juu ya nyumba yake; (na huyu Obadia alikuwa mwenye kumcha Bwana sana;

4kwa kuwa ikawa, Yezebeli alipowaua manabii wa Bwana, Obadia akatwaa manabii mia, akawaficha hamsini hamsini katika pango, akawalisha chakula na kuwapa maji).

5Ahabu akamwambia Obadia, Pita katika nchi, kwenye chemchemi zote za maji, na vijito vyote; labda tutapata majani, tuwahifadhi hai farasi na nyumbu, tusipate hasara ya hao wanyama wote.

6Basi wakaigawanya nchi, ili wapite katika nchi yote; Ahabu akaenda zake njia moja peke yake, na Obadia akaenda zake njia nyingine peke yake.

7Na Obadia alipokuwa njiani, kumbe! Eliya akakutana naye. Akamtambua, akaanguka kifudifudi, akanena, Je! Ni wewe, bwana wangu Eliya?

8Akamjibu, Ni mimi. Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.

9Akamwambia, Nimekosa nini, hata unitie mimi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu, aniue?

10Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, hakuna taifa wala ufalme ambao bwana wangu hakutuma watu wakutafute; na waliposema, Hayupo, akawaapisha ule ufalme, na taifa, ya kwamba hawakukuona.

11Nawe sasa wasema, Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.

12Na itakuwa, mara mimi nikiondoka kwako, roho ya Bwana atakuchukua uende nisikojua; nami nitakapokwenda kumwambia Ahabu, naye asipokuona, ataniua, lakini mimi mtumishi wako namcha Bwana tangu ujana wangu.

13Je! Bwana wangu hakuambiwa nilivyofanya hapo Yezebeli alipowaua manabii wa Bwana? Jinsi nilivyowaficha manabii wa Bwana, watu mia, hamsini hamsini katika pango, nikawalisha chakula na kuwapa maji?

14Nawe sasa wasema, Enenda umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo; basi, ataniua.

15Eliya akasema, Kama Bwana wa majeshi aishivyo ambaye ninasimama mbele zake, hakika nitajionyesha kwake leo.

16Basi, Obadia akaenda zake amwone Ahabu, akamwambia; naye Ahabu akaenda kumlaki Eliya.

17Ikawa, Ahabu alipomwona Eliya, Ahabu akamwambia, Je! Ni wewe, Ewe mtaabishaji wa Israeli?

18Naye akajibu, Si mimi niliyewataabisha Israeli; bali ni wewe, na nyumba ya baba yako, kwa kuwa mmeziacha amri za Bwana; nawe umewafuata mabaali.

19Basi sasa upeleke watu, unikusanyie jamii ya Israeli katika mlima wa Karmeli, na wale manabii wa Baali mia nne na hamsini, na wale manabii wa Ashera mia nne, walao chakula mezani pa Yezebeli.

20Basi, Ahabu akapeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli.

21Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno.

22Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini.

23Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini.

24Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri.

25Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng'ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini.

26Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya.

27Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe.

28Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika.

29Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia.

30Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya Bwana iliyovunjika.

31Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la Bwana na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli.

32Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la Bwana; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu.

33Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng'ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni.

34Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu.

35Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji.

36Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.

37Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.

38Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.

39Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.

40Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko.

41Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele.

42Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini.

43Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba.

44Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie.

45Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli.

46Mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuiingia Yezreeli.