1 Wafalme - Sura ya 22
1Wakakaa miaka mitatu pasipo vita kati ya Shamu na Israeli.
2Ikawa, mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme Wa Yuda akamshukia mfalme wa Israeli.
3Mfalme wa Israeli akawaambia watumishi wake, Je! Hamjui ya kuwa Ramoth-Gileadi ni yetu? Nasi tumenyamaza tusiitwae mkononi mwa mfalme wa Shamu?
4Akamwambia Yehoshafati, Je! Utakwenda nami tupigane na Ramoth-gileadi? Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Mimi ni kama wewe, na watu wangu ni kama watu wako na farasi zangu ni kama farasi zako.
5Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la Bwana.
6Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya pamoja manabii, kama watu mia nne. Akawaambia Je! Niende juu ya Ramoth-Gileadi kuupiga vita, au ninyamaze? Wakasema Kwea; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme.
7Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii wa Bwana tena, ili tumwulize yeye?
8Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza Bwana kwa yeye, yaani Mikaya mwana wa Imla; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema, ila mabaya. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi.
9Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida, akamwambia, mlete hima Mikaya mwana wa Imla.
10Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wakikaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika sakafu langoni pa Samaria; na manabii wote wakafanya unabii mbele yao.
11Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, Bwana asema hivi, Kwa hizo utawasukuma Washami, hata waharibike.
12Na manabii wote wakasema hivyo kwa unabii, wakisema, Kwea Ramoth-Gileadi, ukafanikiwe; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme.
13Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia sasa, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja husema mema kwa mfalme; neno lako na liwe, nakusihi, kama neno la mmojawapo wao, ukaseme mema.
14Mikaya akasema, Kama Bwana aishivyo, neno lile Bwana aniambialo, ndilo nitakalolinena.
15Na alipokuja kwa mfalme, mfalme alimwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-Gileadi kupiga vita, au tunyamaze? Akamwambia, Kwea, ufanikiwe; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme.
16Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la Bwana?
17Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. Bwana akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.
18Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?
19Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto.
20Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.
21Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya.
22Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.
23Basi angalia, Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako.
24Ndipo akakaribia Zedekia, mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Roho ya Bwana alitokaje kwangu ili aseme na wewe?
25Mikaya akamwambia, Angalia, utaona siku ile utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche.
26Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme;
27mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni mtu huyu gerezani, mkamlishe kwa chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani.
28Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, Bwana hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.
29Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-Gileadi.
30Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha, akaingia vitani.
31Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru wakuu wa magari yake thelathini na wawili, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake.
32Ikawa wakuu wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Huyo ndiye mfalme wa Israeli Wakageuka juu yake ili wapigane naye; naye Yehoshafati akapiga ukelele.
33Ikawa, wakuu wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.
34Mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari lake, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.
35Pigano likazidi siku ile; mfalme akategemezwa garini mwake, kinyume cha Washami, hata jioni akafa; damu ikatoka katika jeraha yake ndani ya gari.
36Ikapigwa mbiu jeshini, jua likichwa, kusema, Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake.
37Hivyo akafa mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria.
38Wakaliosha gari penye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake; (basi ndipo walipooga makahaba); sawasawa na neno la Bwana alilolinena.
39Na mambo yote ya Ahabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na nyumba ya pembe aliyoijenga, na miji yote aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
40Basi Ahabu akalala na baba zake; na Ahazia mwanawe akatawala mahali pake.
41Yehoshafati mwana wa Asa alianza kutawala juu ya Yuda, katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli.
42Yehoshafati alikuwa mwenye miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na mitano huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Azuba binti Shilhi.
43Akaiendea njia yote ya Asa babaye; wala hakugeuka, akifanya yaliyo mema machoni pa Bwana. Lakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu wakafukiza uvumba katika mahali pa juu.
44Yehoshafati akafanya amani na mfalme wa Israeli.
45Na mambo yote ya Yehoshafati yaliyosalia, na uthabiti alioufanya, na jinsi alivyopiga vita, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
46Tena mahanithi waliosalia, hao waliosalia siku za Asa baba yake, akawaondoa katika nchi.
47Wala hapakuwa na mfalme katika Edomu; naibu alikuwa ndiye mfalme.
48Yehoshafati akafanya merikebu za Tarshishi ziende Ofiri kuchukua dhahabu; walakini hazikuenda; kwa maana merikebu zilivunjika huko Esion-geberi.
49Ndipo Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, Watumishi wangu na waende pamoja na watumishi wako merikebuni. Lakini Yehoshafati hakukubali.
50Basi Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake; na Yehoramu mwanawe akatawala mahali pake.
51Ahazia mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria, katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akatawala miaka miwili juu ya Israeli.
52Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, akaiendea njia ya babaye, na njia ya mamaye, na njia ya Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli.
53Akamtumikia Baali, akamwabudu, akamghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kwa mfano wa mambo yote aliyoyafanya baba yake.

Swahili
Italiano (it-IT)
Português do Brasil (pt-BR)
Polski (PL)
Deutsch (Deutschland)
Français (France)
Español (España)
Українська Біблія у перекладі Огієнка
English Bible - 21ST CENTURY KING JAMES (KJ21)