1 Wafalme - Sura ya 7

1 Wafalme - Sura ya 7

1Naye Sulemani alikuwa katika kuijenga nyumba yake mwenyewe miaka kumi na mitatu, akaimaliza nyumba yake yote.

2Kwa kuwa aliijenga nyumba ya mwitu wa Lebanoni; mikono mia urefu wake, na mikono hamsini upana wake, na mikono thelathini kwenda juu kwake, juu ya safu nne za nguzo za mwerezi, na mihimili ya mwerezi juu ya nguzo.

3Ikafunikwa juu kwa mwerezi juu ya mihimili arobaini na mitano, iliyokuwa juu ya nguzo; kumi na mitano kwa safu.

4Na madirisha yalikuwako safu tatu, mwangaza kuelekea mwangaza katika madaraja matatu.

5Na milango yote na miimo ilikuwa ya mraba, ilivyoangaziwa; na mwangaza kuelekea mwangaza katika madaraja matatu.

6Akaifanya baraza ya nguzo; mikono hamsini urefu wake, na mikono thelathini upana wake; na ukumbi mbele yake; na nguzo na mihimili minene mbele yake.

7Akaifanya baraza ya kiti cha enzi, ili ahukumu ndani yake, ndiyo baraza ya hukumu; nayo ikafunikwa mwerezi tangu sakafu mpaka dari.

8Nayo nyumba yake atakayokalia, katika behewa nyingine iliyokuwa ndani kupita baraza, ilikuwa ya kazi kama hiyo. Tena akamjengea nyumba binti Farao, (ambaye Sulemani alikuwa amemwoa), mfano wa ile baraza.

9Hizi zote zilikuwa za mawe ya thamani, mawe ya kuchongwa, sawasawa na cheo, yaliyokatwa kwa misumeno, ndani na nje, tangu msingi hata mawe ya juu, na nje vile vile hata behewa kuu.

10Nao msingi ulikuwa wa mawe ya thamani, mawe makubwa, mawe mikono kumi, na mawe ya mikono minane.

11Na juu kulikuwa na mawe ya thamani, mawe ya kuchongwa, sawasawa na cheo, na mierezi.

12Na behewa kubwa pande zote ilikuwa na safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi; mfano wa behewa ya ndani ya nyumba ya Bwana, na ukumbi wa nyumba.

13Mfalme Sulemani akatuma watu kumleta Huramu

14Naye alikuwa mwana wa mwanamke mjane wa kabila ya Naftali, na babaye alikuwa mtu wa Tiro, mfua shaba; naye alikuwa mwingi wa hekima na akili, mstadi wa kufanya kazi zote za shaba. Akamfikilia mfalme Sulemani, akamfanyia kazi yake yote.

15Kwa maana alizifanyiza zile nguzo mbili za shaba, mikono kumi na minane kwenda juu kwake kila moja; na uzi wa mikono kumi na miwili kuizunguka nguzo hii au hii.

16Akafanya taji mbili za shaba iliyoyeyushwa za kuwekwa juu ya vichwa vya nguzo; kwenda juu kwake taji moja mikono mitano, na mikono mitano kwenda juu kwake taji ya pili.

17Kulikuwa na nyavu kama kazi ya kusuka, na masongo ya mikufu, kwa taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; saba kwa taji moja, na saba kwa taji ya pili

18Hivyo akazifanya nguzo; na kulikuwa na safu mbili za kuzunguka juu ya wavu mmoja, zifunike taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; akafanya vivyo hivyo kwa taji ya pili.

19Na taji zilizokuwa juu ya nguzo ukumbini zilikuwa za kazi ya mayungi, mikono minne.

20Kulikuwako tena taji juu ya nguzo mbili, karibu na uvimbe uliokuwako kando ya wavu; na makomamanga yalikuwa mia mbili, safu safu pande zote juu ya taji ya pili.

21Akazisimamisha nguzo ukumbini pa hekalu; akaisimamisha nguzo ya kuume, akaiita jina lake Yakini;

22Na juu ya nguzo kulikuwa na kazi ya mayungi; hivyo mambo ya nguzo yakatimia.

23Tena akaifanya bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ikaviringana, na mikono mitano ilikuwa kwenda juu kwake; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa.

24Na chini ya ukingo wake kulikuwa na maboga yaliyoizunguka, kwa mikono kumi, yakiizunguka bahari; kulikuwa na safu mbili za hayo maboga, yakafanywa kalibuni hapo bahari ilipofanywa.

25Ikakaa juu ya ng'ombe kumi na wawili, watatu wakitazama kaskazini, na watatu wakitazama magharibi, na watatu wakitazama kusini, na watatu wakitazama mashariki; na bahari iliwekwa juu yao, na pande zao za nyuma zote zilikuwa ndani.

26Na unene wake ulikuwa nyanda nne; na ukingo wake ukafanywa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungi; huingia bathi elfu mbili.

27Akayafanya yale matako kumi ya shaba; mikono minne urefu wa tako moja, na mikono minne upana wake, na mikono mitatu kwenda juu kwake.

28Na kazi ya matako ndiyo hii; yalikuwa na papi; na papi zilikuwa katikati ya vipandio;

29na juu ya papi zilizokuwa katikati ya vipandio kulikuwa na simba, na ng'ombe, na makerubi; na juu ya vipandio kulikuwa na tako; na chini ya simba na ng'ombe kulikuwa na masongo ya kazi ya kupembeza.

30Kila tako lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vipini vya shaba; na miguu yake minne ilikuwa na mataruma; chini ya birika yalikuwako mataruma ya kusubu, yenye masongo kila moja mbavuni.

31Na kinywa chake ndani ya taji na juu yake kilikuwa mkono mmoja; na kinywa chake kikaviringana kama kazi ya tako, mkono mmoja na nusu; tena juu ya kinywa chake kulikuwa na nakshi, na papi zao zilikuwa za mraba, wala hazikuviringana.

32Na magurudumu manne yalikuwa chini ya papi; na mikono ya magurudumu ndani ya tako; na kwenda juu kwake gurudumu moja mkono mmoja na nusu.

33Na kazi ya magurudumu ilikuwa kama kazi ya gurudumu la gari; mikono yake, na maduara, na matindi, na vipande vya ndani, vyote vilikuwa vya kusubu.

34Kulikuwa na mataruma manne katika pembe nne za tako moja; mataruma hayo ni kitu kimoja na tako lenyewe.

35Na juu ya tako kulikuwa na duara nusu mkono kwenda juu kwake; na juu ya tako mashikio yake na papi zake vilikuwa vya namna iyo hiyo.

36Akachora juu ya mabamba ya mashikio yake, na juu ya papi zake, makerubi, na simba, na mitende, moja moja kama ilivyokuwa nafasi, na masongo pande zote.

37Hivyo akayafanya yale matako kumi; yote yalikuwa ya kalibu moja, na cheo kimoja, na namna moja.

38Akafanya birika kumi za shaba; birika moja huingia bathi arobaini; na kila birika ilikuwa mikono minne; birika moja juu ya tako moja, katika yale matako kumi.

39Akayaweka yale matako, matano upande wa kuume wa nyumba, na matano upande wa kushoto wa nyumba; akaiweka ile bahari upande wa kuume wa nyumba upande wa mashariki, kuelekea kusini.

40Tena Huramu akazifanya birika, na majembe, na mabakuli. Hivyo Huramu akazimaliza kazi zote alizomfanyia mfalme Sulemani katika nyumba ya Bwana;

41zile nguzo mbili, na vimbe mbili za taji zilikuwa juu ya nguzo; na nyavu mbili za kuzifunika hizo vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo;

42na makomamanga mia nne ya zile nyavu mbili; safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, kuzifunika hizo vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo;

43na yale matako kumi, na birika kumi juu ya matako;

44na ile bahari moja, na ng'ombe kumi na wawili chini ya ile bahari;

45na masufuria, na majembe, na mabakuli; hata vyombo hivyo vyote, Huramu alivyomfanyia mfalme Sulemani, katika nyumba ya Bwana, vyote vilikuwa vya shaba iliyosuguliwa.

46Katika uwanda wa Yordani ndipo mfalme alipovisubu, katika udongo mzito kati ya Sukothi na Sarethani.

47Sulemani akaviacha vyombo vyote visipimwe kwa kuwa vilikuwa vingi mno; wala uzito wa shaba haukujulikana.

48Sulemani akavifanya vyombo vyote vilivyokuwamo nyumbani mwa Bwana; madhabahu ya dhahabu, na ile meza iliyokuwa na mikate ya wonyesho juu yake ilikuwa ya dhahabu;

49na vinara vya taa, vitano upande wa kuume, na vitano upande wa kushoto, mbele ya chumba cha ndani, vya dhahabu safi; na maua, na taa, na koleo ya dhahabu;

50na vikombe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyetezo, vya dhahabu safi; na bawaba za dhahabu, za milango ya nyumba ya ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu, na za milango ya nyumba, ndiyo hekalu.

51Hivyo ikamalizika kazi yote Sulemani mfalme aliyoifanya katika nyumba ya Bwana. Sulemani akaviingiza vile vitu alivyovitakasa Daudi baba yake, yaani, fedha, na dhahabu, na vyombo; akavitia ndani ya hazina za nyumba ya Bwana.