1 Samweli - Sura ya 20

1 Samweli - Sura ya 20

1Kisha Daudi akatoka Nayothi huko Rama, akakimbia, akaenda kwa Yonathani, akasema mbele yake, Nimefanya nini? Uovu wangu ni nini? Dhambi yangu mbele ya baba yako ni nini, hata akaitaka roho yangu?

2Naye akamwambia, Hasha! Hutakufa; angalia, baba yangu hatendi neno kubwa wala dogo bila kuifunulia mimi, na baba yangu ana sababu gani ya kunificha jambo hili? Sivyo usemavyo.

3Daudi akaapa, akasema, Baba yako anajua sana ya kuwa nimeona kibali machoni pako, naye asema, Yonathani asilijue neno hili, asije akahuzunika; lakini ni kweli, aishivyo Bwana, na iishivyo roho yako, iko hatua moja tu kati ya mimi na mauti.

4Ndipo Yonathani akamwambia Daudi, Kadiri roho yako itakavyo, nitakutendea.

5Naye Daudi akamwambia Yonathani, Tazama, kesho ni mwandamo wa mwezi, nami hainipasi kukosa kuketi chakulani pamoja na mfalme; lakini niache nijifiche bondeni hata siku ya tatu jioni.

6Baba yako akiona ya kuwa sipo basi sema, Daudi alitaka sana nimpe ruhusa, aende upesi Bethlehemu, mji wake, kwa maana iko huko dhabihu ya mwaka kwa ajili ya jamaa yake yote.

7Basi, akisema, Ni vema, mimi mtumishi wako nitakuwa na amani; bali akikasirika, ujue ya kuwa amekusudia kutenda jambo baya.

8Basi, unitendee mema mimi mtumishi wako; kwa sababu umenitia mimi mtumishi wako katika agano la Bwana pamoja nawe, lakini ikiwa mna uovu moyoni mwangu, uniue wewe mwenyewe; kwa nini kunileta kwa baba yako?

9Naye Yonathani akasema, Haya na yawe mbali nawe, kwa maana kama ningejua ya kuwa baba yangu amekusudia kukutenda neno baya, je! Singekuambia?

10Basi Daudi akamwambia Yonathani, Ni nani atakayeniambia, ikiwa baba yako amekujibu maneno makali?

11Yonathani akamwambia Daudi, Twende zetu nje mashambani. Wakatoka wote wawili, wakaenda mashambani.

12Naye Yonathani akamwambia Daudi, Bwana, Mungu wa Israeli, na awe shahidi; nitakapokuwa nimekwisha kumwuliza baba yangu, kama wakati huu kesho, au siku ya tatu, angalia, kama liko neno jema la kumfaa Daudi, je! Nisikupelekee habari na kukufunulia neno hili?

13Bwana anitende mimi, Yonathani, hivyo, na kuzidi, ikiwa yampendeza babangu kukutenda mabaya, nisipokufunulia haya, na kukupeleka uende zako kwa amani; na Bwana awe pamoja nawe, kama alivyokuwa pamoja na baba yangu.

14Nawe utanionyesha fadhili za Bwana, ili nisife, si wakati huu tu maadamu mimi ni hai;

15lakini pamoja na hayo, hata jamaa yangu pia hutawaondolea kabisa fadhili zako; la, hata wakati ule Bwana atakapokuwa amewaondoa kabisa adui za Daudi wote pia katika uso wa nchi.

16Basi Yonathani akafanya agano na jamaa yake Daudi, akisema, Bwana naye atayataka mkononi mwa adui zake Daudi.

17Naye Yonathani akamwapisha Daudi mara ya pili, kwa ajili ya upendo aliokuwa nao kwake; kwa maana alimpenda kama alivyoipenda roho yake mwenyewe.

18Kisha Yonathani akamwambia, Kesho ni mwandamo wa mwezi, nawe utakosekana, kwa sababu kiti chako kitakuwa hakina mtu.

19Nawe ukiisha kungoja siku tatu, shuka upesi ufike kuko huko ulikojificha, siku ya shughuli ile; nawe kaa karibu na kile kichuguu kule.

20Nami nitapiga mishale mitatu kando-kando yake, kana kwamba ninapiga shabaha.

21Kisha, angalia, nitamtuma mtoto na kumwambia, Nenda ukaitafute mishale. Hapo nikimwambia yule mtoto, Tazama, mishale iko upande wako huu, itwae; basi uje, maana iko amani kwako, wala hapana hatari, Bwana aishivyo.

22Bali nikimwambia yule mtoto, Tazama, mishale iko huko mbele yako; basi enenda zako, kwa maana Bwana amekuamuru uende zako.

23Na kwa habari ya neno lile tulilonena, wewe na mimi, angalia Bwana yu kati ya wewe na mimi milele.

24Basi Daudi akajificha shambani; na mwezi ulipoandama, mfalme aliketi kula chakula.

25Mfalme aliketi kitini mwake kama sikuzote, katika kiti kilichokuwa karibu na ukuta; Yonathani alikuwa mbele yake; Abneri naye akaketi karibu na Sauli; lakini mahali pake Daudi palikuwa hapana mtu.

26Lakini Sauli hakusema neno siku ile; maana alidhani ya kuwa, Amepatikana na neno, hakutakata; hakosi yeye hakutakata.

27Hata siku ya pili baada ya mwandamo wa mwezi, mahali pake palikuwa hapana mtu; basi Sauli akamwambia Yonathani mwanawe, Mbona mwana wa Yese haji kula chakula, jana wala leo?

28Naye Yonathani akamjibu Sauli, Daudi alitaka sana nimpe ruhusa aende Bethlehemu;

29akasema, Tafadhali nipe ruhusa niende; kwa maana jamaa yetu wana dhabihu mjini mwetu; na ndugu yangu ameniamuru niende; basi sasa, kama nimeona kibali machoni pako, nakuomba, niondoke; nikawatazame ndugu zangu. Ndiyo sababu hakuja mezani pa mfalme.

30Basi hasira yake Sauli ikawaka juu ya Yonathani, akamwambia, Wewe, mwana wa mke mkaidi, asi, je! Mimi sijui ya kuwa umemchagua huyo mwana wa Yese, kwa aibu yako mwenyewe, na kwa aibu ya uchi wa mama yako.

31Maana wakati mwana wa Yese akiwa hai juu ya nchi, wewe hutafanikiwa, wala ufalme wako. Basi, sasa peleka, ukamlete kwangu, maana hakika yake atakufa huyu.

32Yonathani akamjibu Sauli, baba yake, akamwambia, Auawe kwa sababu gani? Amefanya nini?

33Sauli akamtupia mkuki wake ili kumpiga; basi Yonathani akajua ya kuwa baba yake ameazimu kumwua Daudi.

34Basi Yonathani akaondoka pale mezani, mwenye hasira kali, wala hakula chakula siku ya pili ya mwezi, kwa sababu alimhuzunikia Daudi sana, na kwa sababu baba yake amemwaibisha.

35Hata asubuhi Yonathani akatoka kwenda shambani wakati ule alioagana na Daudi, na mtoto mdogo alikuwa pamoja naye.

36Akamwambia mtoto wake, Piga mbio, ukaitafute mishale niipigayo. Na yule mtoto alipokuwa akipiga mbio, akapiga mshale, ukapita juu yake.

37Na mtoto alipofika penye ule mshale alioupiga Yonathani, Yonathani akampigia mtoto kelele, akasema, Je! Mshale si huko mbele yako?

38Yonathani akampigia mtoto kelele, Haya! Hima! Usikawie. Mtoto wa Yonathani akaikusanya mishale, akaenda kwa bwana wake.

39Lakini yule mtoto hakujua lo lote. Yonathani na Daudi ndio walioijua habari yenyewe.

40Naye Yonathani akampa mtoto silaha zake, akamwambia, Nenda, ukazichukue mjini.

41Basi mara alipokuwa amekwisha ondoka yule mtoto, mara Daudi akatoka mahali pale karibu na kile kichuguu, akaanguka kifudifudi, akajiinama mara tatu; nao wakabusiana, wakaliliana, hata Daudi akazidi.

42Naye Yonathani akamwambia Daudi, Enenda kwa amani; kwa maana sisi sote wawili tumeapiana kwa jina la Bwana ya kwamba, Bwana atakuwa kati ya mimi na wewe, na kati ya uzao wangu na uzao wako milele. Daudi akaondoka, akaenda zake; Yonathani naye akaenda zake mjini.