1 Samweli - Sura ya 25

1 Samweli - Sura ya 25

1Akafa Samweli; nao Israeli wote wakakusanyika, wakamwomboleza, wakamzika nyumbani mwake huko Rama.

2Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli.

3Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu.

4Basi Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa katika kuwakata manyoya kondoo zake.

5Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie;

6na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao.

7Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo zako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli.

8Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote kitakachokujia mkononi, uwape watumwa wako na mwanao Daudi.

9Basi walipofika vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali sawasawa na maneno hayo yote kwa jina la Daudi, kisha wakanyamaza.

10Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake!

11Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya kondoo zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi?

12Basi vijana wake Daudi wakageuka, wakaenda zao, wakarudi, nao wakaja wakamwambia sawasawa na maneno hayo yote.

13Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma yake Daudi, wapata kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo vyao.

14Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, kasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana.

15Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako mavueni;

16watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo.

17Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye.

18Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliofanyizwa tayari, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda.

19Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali.

20Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake, na kutelemka penye sitara ya mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa wakishuka kumkabili; naye akawakuta.

21Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu cho chote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema.

22Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi.

23Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi.

24Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.

25Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma.

26Basi sasa, bwana wangu, aishivyo Bwana, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa Bwana amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali.

27Na sasa zawadi hii, mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu.

28Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika Bwana atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya Bwana; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote.

29Na hata ijapokuwa binadamu angeinuka akuwinde, na kuitafuta nafsi yako, hiyo nafsi ya bwana wangu itafungwa katika furushi ya uhai pamoja na Bwana, Mungu wako; na nafsi za adui zako ndizo atakazozitupa nje, kama kutoka kati ya teo.

30Tena itakuwa, hapo Bwana atakapokuwa amemtendea bwana wangu sawasawa na mema yote aliyoyanena juu yako, na kukutawaza juu ya Israeli;

31hili halitakuwa kwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu, ama ya kuwa umemwaga damu bure, ama ya kuwa bwana wangu amejilipiza kisasi mwenyewe; tena hapo Bwana atakapokuwa amemtendea bwana wangu mema, ndipo umkumbuke mjakazi wako.

32Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki;

33na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe.

34Kwa kuwa ni kweli, aishivyo Bwana, Mungu wa Israeli, aliyenizuia nisikudhuru, kwamba hungefanya haraka kuja kunilaki, hakika huyu Nabali asingaliachiwa hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi.

35Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea; akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimeukubali uso wako.

36Kisha Abigaili alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake, kama karamu ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa maana amelewa kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hata kulipopambazuka.

37Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe alimwambia mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe.

38Tena ikawa, yapata siku kumi baadaye, Bwana alimpiga huyo Nabali, hata akafa.

39Naye aliposikia ya kwamba Nabali amekufa, Daudi alisema, Na ahimidiwe Bwana ambaye amenitetea teto la shutumu langu mkononi mwa Nabali, na kumzuia mtumwa wake asitende maovu; tena uovu wake Nabali Bwana amemrudishia juu ya kichwa chake mwenyewe. Kisha Daudi akatuma watu, akamposa Abigaili ili amwoe.

40Na hao watumishi wa Daudi walipomjia huyo Abigaili huko Karmeli, walimwambia, wakasema, Daudi ametutuma kwako ili tukutwae uwe mkewe.

41Naye akainuka na kujiinamisha kifulifuli mpaka nchi, akasema, Tazama, mjakazi wako ni mtumwa wa kuwaosha miguu watumishi wa bwana wangu.

42Abigaili akafanya haraka, akainuka, akapanda punda, pamoja na vijakazi watano wake waliofuatana naye, akawafuata hao wajumbe wa Daudi, akawa mkewe.

43Tena Daudi akamwoa Ahinoamu wa Yezreeli; wakawa wote wawili wakeze.

44Walakini Sauli alikuwa amempa Palti, mwana wa Laishi, aliyekuwa mtu wa Galimu, Mikali binti yake, aliyekuwa mkewe Daudi.