1 Wathesalonike - Sura ya 2

1 Wathesalonike - Sura ya 2

1Maana ninyi wenyewe, ndugu, mwakujua kuingia kwetu kwenu, ya kwamba hakukuwa bure;

2lakini tukiisha kuteswa kwanza na kutendwa jeuri, kama mjuavyo, katika Filipi, twalithubutu katika Mungu kuinena Injili ya Mungu kwenu, kwa kuishindania sana.

3Kwa maana maonyo yetu siyo ya ukosefu, wala ya uchafu, wala ya hila;

4bali kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu anayetupima mioyo yetu.

5Maana hatukuwa na maneno ya kujipendekeza wakati wo wote, kama mjuavyo, wala maneno ya juujuu ya kuficha choyo; Mungu ni shahidi.

6Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine tulipokuwa tukiweza kuwalemea kama mitume wa Kristo;

7bali tulikuwa wapole katikati yenu, kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe.

8Vivyo hivyo nasi tukiwatumaini kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu.

9Maana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu.

10Ninyi ni mashahidi, na Mungu pia, jinsi tulivyokaa kwenu ninyi mnaoamini, kwa utakatifu, na kwa haki, bila kulaumiwa;

11vile vile, kama mjuavyo, jinsi tulivyomwonya kila mmoja wenu kama baba awaonyavyo watoto wake mwenyewe, tukiwatia moyo na kushuhudia;

12ili mwenende kama ilivyo wajibu wenu kwa Mungu, mwenye kuwaita ninyi ili mwingie katika ufalme wake na utukufu wake.

13Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.

14Maana ninyi, ndugu, mlikuwa wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyo katika Uyahudi, katika Kristo Yesu; kwa kuwa mlipata mateso yale yale kwa watu wa taifa lenu wenyewe, waliyoyapata na hao kwa Wayahudi;

15ambao walimwua Bwana Yesu, na hao manabii, na kutuudhi sisi; wala hawampendezi Mungu, wala hawapatani na watu wo wote;

16huku wakituzuia tusiseme na Mataifa wapate kuokolewa; ili watimize dhambi zao siku zote. Lakini hasira imewafikia hata mwisho.

17Lakini sisi, ndugu, tukiwa tumefarakana nanyi kwa kitambo, kwa uso si kwa moyo, tulizidi kutamani kwa shauku nyingi kuwaona nyuso zenu.

18Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia.

19Maana tumaini letu, au furaha yetu, au taji ya kujionea fahari, ni nini? Je! Si ninyi, mbele za Bwana wetu Yesu, wakati wa kuja kwake?

20Maana ninyi ndinyi utukufu wetu, na furaha yetu.