1 Wathesalonike - Sura ya 3

1Basi kwa hiyo, tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliona vema kuachwa Athene peke yetu.
2Tukamtuma Timotheo ndugu yetu, mtumishi wa Mungu katika Injili ya Kristo, ili kuwafanya ninyi imara na kuwafariji kwa habari ya imani yenu;
3mtu asifadhaishwe na dhiki hizi; maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa twawekewa hizo.
4Kwa kuwa tulipokuwapo kwenu tulitangulia kuwaambia kwamba tutapata dhiki, kama ilivyotukia, nanyi mwajua.
5Kwa hiyo mimi nami nilipokuwa siwezi kuvumilia tena, nalituma mtu ili niijue imani yenu, asije yule mjaribu akawajaribu, na taabu yetu ikawa haina faida.
6Lakini Timotheo alipotujia hivi sasa kutoka kwenu, alituletea habari njema za imani yenu na upendo wenu, na ya kwamba mnatukumbuka vema siku zote; mkitamani kutuona sisi vile vile kama sisi kuwaona ninyi.
7Kwa sababu hiyo, ndugu, tulifarijiwa kwa habari zenu, katika msiba na dhiki yetu yote, kwa imani yenu.
8Kwa kuwa sasa twaishi, ikiwa ninyi mnasimama imara katika Bwana.
9Maana ni shukrani gani tuwezayo kumlipa Mungu kwa ajili yenu, kwa furaha ile yote tunayoifurahia, kwa sababu yenu mbele za Mungu wetu;
10usiku na mchana tunapoomba kwa juhudi tupate kuwaona nyuso zenu, na kuyatengeneza mapungufu ya imani yenu?
11Basi Mungu mwenyewe, Baba yetu, na Bwana wetu Yesu, atuongoze njia yetu tufike kwenu.
12Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu;
13apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote.