1 Wathesalonike - Sura ya 4

1 Wathesalonike - Sura ya 4

1Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana.

2Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu.

3Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati;

4kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;

5si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu.

6Mtu asimpunje ndugu yake wala kumkosa katika jambo hili; kwa sababu Bwana ndiye alipizaye kisasi cha haya yote; kama tulivyowaambia kwanza, tukashuhudia sana.

7Maana Mungu hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso.

8Basi yeye anayekataa, hakatai mwanadamu bali Mungu, anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.

9Katika habari ya upendano, hamna haja niwaandikie; maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.

10Kwa maana mnafanya neno hili kwa ndugu wote walio katika Makedonia yote. Lakini twawasihi, ndugu, mzidi sana.

11Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaagiza;

12ili mwenende kwa adabu mbele yao walio nje, wala msiwe na haja ya kitu cho chote.

13Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini.

14Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye.

15Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti.

16Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.

17Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.

18Basi, farijianeni kwa maneno hayo.