1 Wathesalonike - Sura ya 5

1 Wathesalonike - Sura ya 5

1Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.

2Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.

3Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.

4Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.

5Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.

6Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.

7Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.

8Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.

9Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate wokovu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo;

10ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, kwamba twakesha au kwamba twalala.

11Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya.

12Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni;

13mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi.

14Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote.

15Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.

16Furahini siku zote;

17ombeni bila kukoma;

18shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.

19Msimzimishe Roho;

20msitweze unabii;

21jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema;

22jitengeni na ubaya wa kila namna.

23Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.

24Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya.

25Ndugu, tuombeeni.

26Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu.

27Nawaapisha kwa Bwana, ndugu wote wasomewe waraka huu.

28Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi.