1 Timotheo - Sura ya 2

1 Timotheo - Sura ya 2

1Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote;

2kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.

3Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu;

4ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.

5Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;

6ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.

7Nami kwa ajili ya huo naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli.

8Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.

9Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

10bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.

11Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.

12Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu.

13Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.

14Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.

15Walakini ataokolewa kwa uzazi wake, kama wakidumu katika imani na upendo na utakaso, pamoja na moyo wa kiasi.