1 Timotheo - Sura ya 4

1 Timotheo - Sura ya 4

1Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;

2kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;

3wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.

4Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani;

5kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.

6Uwakumbushe ndugu mambo hayo, nawe utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, na mzoevu wa maneno ya imani, na mafundisho mazuri yale uliyoyafuata.

7Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa.

8Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye.

9Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa;

10kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio.

11Mambo hayo uyaagize na kuyafundisha.

12Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.

13Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha.

14Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee.

15Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote.

16Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.