1 Timotheo - Sura ya 6

1 Timotheo - Sura ya 6

1Wo wote walio chini ya kongwa, hali ya utumwa, na wawahesabie bwana zao kuwa wamestahili heshima yote, jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu.

2Na wale walio na bwana waaminio wasiwadharau kwa kuwa ni ndugu; bali afadhali wawatumikie, kwa sababu hao waishirikio faida ya kazi yao wamekuwa wenye imani na kupendwa. Mambo hayo uyafundishe na kuonya.

3Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa,

4amejivuna; wala hafahamu neno lo lote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo hutoka husuda, na ugomvi, na matukano, na shuku mbaya;

5na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida.

6Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa.

7Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu;

8ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.

9Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.

10Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.

11Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole.

12Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi.

13Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato,

14kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo;

15ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana;

16ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina.

17Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha.

18Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo;

19huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli.

20Ee Timotheo, ilinde hiyo amana; ujiepushe na maneno yasiyo ya dini, yasiyo na maana, na mashindano ya elimu iitwayo elimu kwa uongo;

21ambayo wengine wakiikiri hiyo wameikosa Imani. Neema na iwe pamoja nanyi.