2 Mambo ya Nyakati - Sura ya 15

2 Mambo ya Nyakati - Sura ya 15

1Ndipo roho ya Mungu ikamjia Azaria mwana wa Odedi;

2naye akatoka ili amlaki Asa, akamwambia, Nisikieni, Ee Asa, na Yuda wote na Benyamini; Bwana yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi.

3Basi tangu siku nyingi Israeli wamekuwa hawana Mungu wa kweli, wala hawana kuhani afundishaye, wala hawana torati;

4lakini walipomgeukia Bwana, Mungu wa Israeli, katika msiba wao, na kumtafuta, akaonekana kwao.

5Hata na zamani zile hakukuwa na amani kwake atokaye, wala kwake aingiaye, ila fadhaa kubwa juu yao wote wakaao katika nchi.

6Wakavunjika-vunjika, taifa juu ya taifa, na mji juu ya mji; kwani Mungu aliwafadhaisha kwa shida zote.

7Nanyi jipeni nguvu, wala mikono yenu isilegee; kwa maana kazi yenu itakuwa na ijara.

8Naye Asa alipoyasikia maneno hayo, yaani, unabii wa mwana wa Odedi nabii, akatiwa nguvu, akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi ya Yuda na Benyamini, na katika miji aliyoitwaa milimani mwa Efraimu; akaifanyiza tena madhabahu ya Bwana, iliyokuwako mbele ya ukumbi wa Bwana.

9Akakusanya Yuda wote na Benyamini, na hao wageni waliokaa kwao, wa Efraimu, na wa Manase, na wa Simeoni; kwa kuwa walimwangukia wengi katika Israeli, walipoona kwamba Bwana, Mungu wake, alikuwa pamoja naye.

10Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu, katika mwaka wa kumi na tano wa kumiliki kwake Asa.

11Wakamchinjia Bwana siku ile, katika nyara walizozileta, dhabihu za ng'ombe mia saba, na kondoo elfu saba.

12Wakafanya agano, ya kuwa watamtafuta Bwana, Mungu wa baba zao, kwa mioyo yao yote, na kwa roho zao zote;

13na ya kwamba ye yote asiyemtafuta Bwana, Mungu wa Israeli, atauawa, akiwa mdogo au mkubwa, kwamba ni mwanamume au mwanamke.

14Wakamwapia Bwana kwa sauti kuu, na kwa kelele, na kwa mapanda, na kwa baragumu.

15Na Yuda wote wakakifurahia kile kiapo; kwani wameapa kwa moyo wao wote, na kumtafuta kwa mapenzi yao pia; naye ameonekana kwao; naye Bwana akawastarehesha pande zote.

16Hata na Maaka mamaye Asa, mfalme akamwondolea daraja yake asiwe malkia, kwa kuwa amefanya sanamu ya kuchukiza kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake, akaiponda, akaiteketeza penye kijito cha Kidroni.

17Lakini mahali pa juu hapakuondolewa katika Israeli; ila moyo wake Asa ulikuwa mkamilifu siku zake zote.

18Akavileta nyumbani mwa Mungu vitu alivyovitakasa babaye, na vile alivyovitakasa mwenyewe, fedha, na dhahabu, na vyombo.

19Wala hapakuwa na vita tena hata mwaka wa thelathini na tano wa kutawala kwake Asa.