2 Mambo ya Nyakati - Sura ya 19

2 Mambo ya Nyakati - Sura ya 19

1Yehoshafati mfalme wa Yuda akarudi Yerusalemu nyumbani kwake kwa amani.

2Yehu mwana wa Hanani mwonaji akatoka kwenda kumlaki, akamwambia mfalme Yehoshafati, Je! Imekupasa kuwasaidia waovu, na kuwapenda wamchukiao Bwana? Kwa ajili ya hayo ghadhabu i juu yako itokayo kwa Bwana.

3Walakini yameonekana mema ndani yako, kwa kuwa umeyaondoa maashera katika nchi, na moyo wako umeukaza kumtafuta Mungu.

4Na Yehoshafati akakaa Yerusalemu; akatoka tena kwenda kati ya watu toka Beer-sheba mpaka milima ya Efraimu, akawarudisha kwa Bwana, Mungu wa baba zao.

5Akasimamisha makadhi katika nchi, katikati ya miji yote yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji;

6akawaambia hao makadhi, Angalieni myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila Bwana; naye yupo pamoja nanyi katika neno la hukumu.

7Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu; angalieni mkaifanye; kwa maana kwa Bwana, Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za watu, wala kupokea zawadi.

8Tena katika Yerusalemu Yehoshafati akasimamisha wa Walawi na makuhani, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli wawe kwa hukumu ya Bwana, na kwa mateto. Nao wakarudi Yerusalemu.

9Akawaagiza, akasema, Ndivyo mtakavyotenda kwa hofu ya Bwana, kwa uaminifu, na kwa moyo kamili.

10Na kila mara watakapowajia na teto ndugu zenu wakaao mijini mwao, kati ya damu na damu, kati ya torati na amri, sheria na hukumu, mtawaonya, wasiingie hatiani mbele za Bwana, mkajiliwa na ghadhabu ninyi na ndugu zenu; fanyeni haya wala hamtakuwa na hatia.

11Tena angalieni, Amaria, kuhani mkuu, yu juu yenu kwa maneno yote ya Bwana; naye Zebadia, mwana wa Ishmaeli, jemadari wa nyumba ya Yuda, kwa maneno yote ya mfalme; Walawi nao watakuwa wasimamizi mbele yenu. Jitieni nguvu, mtende, naye Bwana awe pamoja nao walio wema.