2 Mambo ya Nyakati - Sura ya 21

2 Mambo ya Nyakati - Sura ya 21

1Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; akatawala Yehoramu mwanawe mahali pake.

2Naye alikuwa na ndugu, wana wa Yehoshafati, Azaria, na Yehieli, na Zekaria, na Azaria, na Mikaeli, na Shefatia; hao wote walikuwa wana wa Yehoshafati mfalme wa Israeli.

3Baba yao akawapa zawadi kubwa, za fedha, na za dhahabu, na za tunu, pamoja na miji yenye maboma katika Yuda; lakini ufalme akampa Yehoramu, kwa sababu alikuwa mzaliwa wa kwanza.

4Basi Yehoramu alipoinuliwa juu ya ufalme wa babaye, na kujitia nguvu, akawaua nduguze wote kwa upanga, na baadhi ya wakuu wa Israeli pia.

5Yehoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala miaka minane huko Yerusalemu.

6Akaiendea njia ya wafalme wa Israeli, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; kwa kuwa alikuwa amemwoa binti Ahabu; akafanya maovu machoni pa Bwana.

7Walakini Bwana hakupenda kuiharibu nyumba ya Daudi, kwa sababu ya agano alilolifanya na Daudi, na kama alivyomwahidi kuwa atampa taa, yeye na wazao wake siku zote.

8Zamani zake Edomu wakaasi chini ya mkono wa Yuda, wakajifanyia mfalme.

9Ndipo akavuka Yehoramu na maakida wake, na magari yake yote pamoja naye; akaondoka usiku, akawapiga Waedomi waliomzunguka yeye na hao maakida wa magari.

10Hivyo Edomu wakaasi chini ya mkono wa Yuda, hata leo; wakaasi na Libna zamani zizo hizo chini ya mkono wake: kwa sababu alikuwa amemwacha Bwana, Mungu wa baba zake.

11Tena ndiye aliyefanya mahali pa juu milimani pa Yuda, na kuwaendesha katika uasherati wenyeji wa Yerusalemu, na kuwakosesha Yuda.

12Likamjia andiko kutoka kwa Eliya nabii, kusema, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako, asema hivi, Kwa sababu hukuziendea njia za Yehoshafati baba yako, wala njia za Asa mfalme wa Yuda;

13lakini umeiendea njia ya wafalme wa Israeli, ukawaendesha katika uasherati Yuda na wenyeji wa Yerusalemu, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; tena umewaua ndugu zako wa nyumba ya baba yako, waliokuwa wema kuliko wewe;

14tazama, Bwana atawapiga pigo kubwa watu wako, na watoto wako, na wake zako, na mali yako yote;

15nawe utakuwa na ugonjwa mkuu kwa maradhi ya matumbo, yatakapotokea matumbo yako kwa sababu ya ugonjwa huo siku kwa siku.

16Bwana akawaamsha roho Wafilisti, na Waarabu waliowaelekea Wakushi juu ya Yehoramu,

17nao wakakwea juu ya nchi ya Yuda, wakaipenya, wakaichukua mali yote iliyoonekama nyumbani mwa mfalme, na wanawe pia, na wakeze; asisaziwe mwana hata mmoja, ila Ahazia,

18Na baada ya hayo yote Bwana akampiga matumbo kwa ugonjwa usioponyeka.

19Ikawa baada ya siku, ikiisha miaka miwili, matumbo yake yakatokea kwa sababu ya ugonjwa wake, akafa akiugua vibaya. Wala watu wake hawakumfukizia mafukizo kama ya baba zake.

20Alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu miaka minane; akafariki bila kutamaniwa; wakamzika mjini mwa Daudi, ila si katika makaburi ya wafalme.