2 Mambo ya Nyakati - Sura ya 23

1Hata mwaka wa saba Yehoyada akajitia nguvu, akawatwaa maakida wa mamia, Azaria mwana wa Yerohamu, na Ishmaeli mwana wa Yehohanani, na Azaria mwana wa Obedi, na Maaseya mwana wa Adaya, na Elishafati mwana wa Zikri, akapatana nao.
2Wakazunguka katikati ya Yuda, wakawakusanya Walawi kutoka katika miji yote ya Yuda, na wakuu wa nyumba za mababa wa Israeli, wakaja Yerusalemu.
3Na kusanyiko lote wakafanya agano na mfalme nyumbani mwa Mungu. Akawaambia, Angalieni, mwana wa mfalme atatawala, kama Bwana alivyonena juu ya wana wa Daudi.
4Hili ndilo neno mtakalolifanya; theluthi yenu, ninyi mwingiao siku ya sabato, wa makuhani, na wa Walawi, mtalinda milangoni;
5na theluthi nyumbani pa mfalme; na theluthi mlangoni pa msingi; na watu wote watakuwapo nyuani mwa nyumba ya Bwana.
6Wala asiingie mtu nyumbani mwa Bwana, ila makuhani, na hao watumikao wa Walawi; hao wataingia, kwa kuwa hao ni watakatifu; ila watu wote watalinda malinzi ya Bwana.
7Nao Walawi watamzunguka mfalme pande zote, kila mtu mwenye silaha zake mkononi; naye awaye yote aingiaye nyumbani na auawe; nanyi mfuatane na mfalme, aingiapo na atokapo.
8Basi Walawi na Yuda wote wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia siku ya sabato, na wale watakaotoka siku ya sabato; kwa maana Yehoyada kuhani hakuzifumua zamu.
9Naye Yehoyada kuhani akawapa maakida wa mamia mikuki, na ngao, na vigao, vilivyokuwa vya mfalme Daudi, vilivyokuwamo nyumbani mwa Mungu.
10Akawasimamisha watu wote, kila mtu mwenye silaha yake mkononi, toka pembe ya kuume ya nyumba mpaka pembe ya kushoto, upande wa madhabahu na nyumba, kumzunguka mfalme pande zote.
11Ndipo wakamleta nje mwana wa mfalme, wakamvika taji, na kumpa ule ushuhuda, wakamtawaza awe mfalme; Yehoyada na wanawe wakamtia mafuta, wakasema, Mfalme na aishi.
12Na Athalia alipoisikia sauti ya watu, na ya walinzi, na ya hao waliomsifu mfalme, akaingia kwa watu nyumbani mwa Bwana;
13akatazama, na angalia, mfalme amesimama karibu na nguzo yake mlangoni, nao maakida na wenye mapanda karibu na mfalme; wakafurahi watu wote wa nchi, wakapiga mapanda; waimbaji pia wakipiga vinanda, wakaongoza nyimbo za kusifu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akasema, Fitina! Fitina!
14Yehoyada kuhani akawaleta nje maakida wa mamia, waliowekwa juu ya jeshi, akawaambia, Mtoeni nje kati ya safu; naye ye yote amfuataye, na auawe kwa upanga; kwani kuhani amesema, Msimwue katika nyumba ya Bwana.
15Basi wakampisha njia; akaenda kwa kuingia pa mlango wa farasi nyumbani mwa mfalme; nao wakamwua huko.
16Kisha, Yehoyada akafanya agano, yeye na watu wote, na mfalme, kwamba watakuwa watu wa Bwana.
17Na watu wote wakaiendea nyumba ya Baali, wakaibomoa; wakavunja-vunja madhabahu zake na sanamu zake, wakamwua Matani kuhani wa Baali mbele ya madhabahu.
18Yehoyada akauamuru usimamizi wa nyumba ya Bwana chini ya mkono wa makuhani Walawi, aliowagawa Daudi nyumbani mwa Bwana, ili wazisongeze sadaka za kuteketezwa za Bwana, kama ilivyoandikwa katika torati ya Musa, kwa kufurahi na kuimba, kama alivyoamuru Daudi.
19Akawasimamisha walinzi malangoni pa nyumba ya Bwana, asiingie aliye mchafu kwa vyo vyote.
20Akawatwaa maakida wa mamia, na watu wakubwa, na hao watawalao watu, na watu wote wa nchi, akamtelemsha mfalme kutoka nyumba ya Bwana; wakalipitia lango la juu waende nyumbani kwa mfalme, wakamketisha mfalme katika kiti cha ufalme.
21Basi wakafurahi watu wote wa nchi, na mji ukatulia; naye Athalia wakamwua kwa upanga.