2 Mambo ya Nyakati - Sura ya 30
1Hezekia akatuma wajumbe kwa Israeli wote na Yuda pia; akawaandikia nyaraka Efraimu na Manase, waje nyumbani kwa Bwana Yerusalemu, ili wamfanyie pasaka Bwana, Mungu wa Israeli.
2Kwa maana mfalme na wakuu wake, na kusanyiko lote katika Yerusalemu walifanya shauri kufanya pasaka mwezi wa pili.
3Kwa sababu hawakuweza kuifanya wakati ule, kwa kuwa makuhani walikuwa hawajajitakasa wa kutosha, wala watu hawajakusanyika huko Yerusalemu.
4Likawa neno jema machoni pa mfalme, na kusanyiko lote.
5Basi wakafanya amri kupiga mbiu kati ya Israeli yote, toka Beer-sheba mpaka Dani, ya kwamba watu waje wamfanyie pasaka Bwana, Mungu wa Israeli, huko Yerusalemu; maana tangu siku nyingi hawakuifanya kama vile ilivyoandikwa.
6Wakaenda matarishi wenye nyaraka za mfalme na wakuu wake, kati ya Israeli yote na Yuda, na kwa amri ya mfalme, kusema, Enyi wana wa Israeli, mrudieni Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, apate kuwarudia waliosalia wenu waliookoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru.
7Wala msiwe kama baba zenu, na kama ndugu zenu, waliomwasi Bwana, Mungu wa baba zao, hata akawatoa kuwa ushangao, kama mwonavyo.
8Msiwe sasa wenye shingo ngumu kama baba zenu; lakini mjitoe kwa Bwana, mkaingie katika patakatifu pake, alipopatakasa milele, mkamtumikie Bwana, Mungu wenu, hasira yake kali iwageukie mbali.
9Kwa kuwa mkimrudia Bwana, ndugu zenu na watoto wenu watahurumiwa machoni pa hao waliowachukua mateka, nao watairudia nchi hii; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye mwenye neema, na mwenye rehema, wala hatawageuzia mbali uso wake, mkimrudia.
10Basi matarishi wakapita mji kwa mji kati ya nchi ya Efraimu na Manase, hata kufika Zabuloni; lakini waliwacheka-cheka, na kuwadhihaki.
11Ila watu wengine wa Asheri, na wa Manase, na wa Zabuloni walijinyenyekeza, wakaja Yerusalemu.
12Tena katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa ukiwapa moyo mmoja, waitimize amri ya mfalme na wakuu kwa neno la Bwana.
13Basi wakakusanyika Yerusalemu watu wengi ili kuifanya sikukuu ya mikate isiyochachwa katika mwezi wa pili, kusanyiko kuu sana.
14Wakainuka, wakaziondoa madhabahu zilizokuwamo Yerusalemu, nazo madhabahu za kufukizia wakaziondoa, wakazitupa katika kijito Kidroni.
15Kisha wakaichinja pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili, nao makuhani na Walawi wakatahayarika, wakajitakasa, wakaleta sadaka za kuteketezwa nyumbani mwa Bwana.
16Wakasimama mahali pao kwa taratibu yao, sawasawa na torati ya Musa, mtu wa Mungu; nao makuhani wakainyunyiza damu, waliyoipokea mikononi mwa Walawi.
17Kwa maana kulikuwa na wengi katika kusanyiko ambao hawajajitakasa; kwa hiyo Walawi wakamchinjia pasaka, kila mtu asiyekuwa safi, ili kuwatakasa kwa Bwana.
18Kwani wingi wa watu, naam, wengi wa Efraimu, na wa Manase, na wa Isakari, na wa Zabuloni, hawakujisafisha, lakini wakala pasaka, ila si kama ilivyoandikwa. Naye Hezekia alikuwa amewaombea, akisema, Bwana mwema na amsamehe kila mtu,
19aukazaye moyo wake kumtafuta Mungu, Bwana, Mungu wa babaze, hata ikiwa si kwa utakaso wa patakatifu.
20Bwana akamsikia Hezekia, akawaponya watu.
21Nao wana wa Israeli waliohudhuria Yerusalemu wakafanya sikukuu ya mikate isiyochachwa siku saba kwa furaha kubwa; Walawi na makuhani wakamsifu Bwana siku kwa siku, wakimwimbia Bwana kwa vinanda vyenye sauti kuu.
22Hezekia akawafurahisha mioyo Walawi wote waliokuwa wastadi wa kumtumikia Bwana. Basi muda wa siku saba wakala sikukuu, wakitoa dhabihu za sadaka za amani, na kumtolea shukrani Bwana, Mungu wa baba zao.
23Na kusanyiko lote wakafanya shauri kufanya sikukuu siku saba nyingine; wakafanya sikukuu siku saba nyingine kwa furaha.
24Maana Hezekia, mfalme wa Yuda, aliwatolea kusanyiko matoleo ya ng'ombe elfu, na kondoo elfu saba; na wakuu wakawatolea kusanyiko ng'ombe elfu, na kondoo elfu kumi; tena wakajitakasa makuhani wengi sana.
25Na kusanyiko lote la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi, na kusanyiko lote waliotoka Israeli, na wageni waliotoka katika nchi ya Israeli, nao waliokaa Yuda, wakafurahi.
26Ikawa furaha kuu katika Yerusalemu; kwa sababu tangu siku za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli, hayajakuwako mambo kama hayo huko Yerusalemu.
27Ndipo wakasimama makuhani Walawi, wakawabariki watu; ikasikiwa sauti yao, sala yao ikafika hata makao yake matakatifu, yaani, mbinguni.

Swahili
Italiano (it-IT)
Português do Brasil (pt-BR)
Polski (PL)
Deutsch (Deutschland)
Français (France)
Español (España)
Українська Біблія у перекладі Огієнка
English Bible - 21ST CENTURY KING JAMES (KJ21)