2 Wakorinto - Sura ya 11

2 Wakorinto - Sura ya 11

1Laiti mngechukuliana nami katika upumbavu wangu kidogo! Naam, mchukuliane nami.

2Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.

3Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.

4Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye!

5Maana nadhani ya kuwa mimi sikupungukiwa na kitu walicho nacho mitume walio wakuu.

6Lakini nijapokuwa mimi ni mtu asiyejua kunena, hii si hali yangu katika elimu; ila katika kila neno tumedhihirishwa kwenu.

7Je! Nalifanya dhambi kwa kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwahubiri Injili ya Mungu bila ujira?

8Naliwanyang'anya makanisa mengine mali yao, nikitwaa posho langu ili niwahudumie ninyi.

9Nami nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana hao ndugu waliokuja kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu; nami katika mambo yote najilinda nafsi yangu nisiwalemee hata kidogo; tena najilinda.

10Kama vile ile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu atakayenifumba kinywa katika kujisifu huku, katika mipaka ya Akaya.

11Kwa nini? Je! Ni kwa sababu siwapendi ninyi? Mungu anajua.

12Lakini nifanyalo nitalifanya, ili niwapinge hao watafutao nafasi wasipate nafasi; ili kwamba katika neno hilo wajisifialo waonekane kuwa kama sisi.

13Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo.

14Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.

15Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.

16Nasema tena, mtu asidhani ya kuwa mimi ni mpumbavu; lakini mjaponidhania hivi, mnikubali kama mpumbavu; ili mimi nami nipate kujisifu ngaa kidogo.

17Ninenalo silineni agizo la Bwana, bali kama kwa upumbavu, katika ujasiri huu wa kujisifu.

18Kwa sababu wengi wanajisifu kwa jinsi ya mwili, mimi nami nitajisifu.

19Ninyi, kwa kuwa mna akili, mnachukuliana na wajinga kwa furaha.

20Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni.

21Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Walakini, akiwa mtu anao ujasiri kwa lo lote, (nanena kipuuzi), mimi nami ninao ujasiri.

22Wao ni Waebrania? Na mimi pia. Wao ni Waisraeli? Na mimi pia. Wao ni uzao wa Ibrahimu? Na mimi pia.

23Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi.

24Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja.

25Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini;

26katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo;

27katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi.

28Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote.

29Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe?

30Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu.

31Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo.

32Huko Dameski liwali wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, ili kunikamata;

33nami nikatelemshwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka katika mikono yake.