2 Wakorinto - Sura ya 12

2 Wakorinto - Sura ya 12

1Sina budi kujisifu, ijapokuwa haipendezi; lakini nitafikilia maono na mafunuo ya Bwana.

2Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu.

3Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua);

4ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene.

5Kwa habari za mtu kama huyo nitajisifu; lakini kwa ajili ya nafsi yangu sitajisifu, isipokuwa katika habari ya udhaifu wangu.

6Maana kama ningetaka kujisifu singekuwa mpumbavu, kwa sababu nitasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu asinihesabie zaidi ya hayo ayaonayo kwangu au kuyasikia kwangu.

7Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi.

8Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke.

9Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.

10Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.

11Nimekuwa mpumbavu, ninyi mmenilazimisha. Maana ilinipasa nisifiwe na ninyi; kwa sababu sikuwa duni ya mitume walio wakuu kwa lo lote, nijapokuwa si kitu.

12Kweli ishara za mtume zilitendwa katikati yenu katika saburi yote, kwa ishara na maajabu na miujiza.

13Maana ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila kwa kuwa mimi sikuwalemea? Mnisamehe udhalimu huu.

14Tazama, hii ni mara ya tatu ya mimi kuwa tayari kuja kwenu, wala sitawalemea. Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi; maana haiwapasi watoto kuweka akiba kwa wazazi, bali wazazi kwa watoto.

15Nami kwa furaha nyingi nitatapanya, tena nitatapanywa kwa ajili ya roho zenu. Je! Kadiri nizidivyo kuwapenda sana, ninapungukiwa kupendwa?

16Lakini na iwe hivyo, mimi sikuwalemea; bali kwa kuwa mwerevu naliwapata kwa hila.

17Je! Mtu ye yote niliyemtuma kwenu, kwa mtu huyo naliwatoza kitu?

18Nalimwonya Tito, nikamtuma ndugu yule pamoja naye. Je! Tito aliwatoza kitu? Je! Hatukuenenda kwa Roho yeye yule na katika nyayo zile zile?

19Mwadhani hata sasa ya kuwa najidhuru kwenu! Mbele za Mungu twanena katika Kristo. Na hayo yote, wapenzi, ni kwa ajili ya kuwajenga ninyi.

20Maana nachelea, nisije nikawakuta si kama vile nitakavyo kuwakuta, nikaonekana kwenu si kama vile mtakavyo; nisije nikakuta labda fitina na wivu, na ghadhabu, na ugomvi, na masingizio, na manong'onezo, na majivuno, na ghasia;

21nami nitakapokuja tena, Mungu wangu asije akanidhili kwenu, nami nikawasikitikia wengi waliokosa tangu hapo, wasiutubie uchafu, na uasherati, na ufisadi walioufanya.