2 Wafalme - Sura ya 23

2 Wafalme - Sura ya 23

1Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu.

2Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa Bwana, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana katika nyumba ya Bwana.

3Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za Bwana, kumfuata Bwana, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile.

4Kisha, mfalme akamwamuru Hilkia, kuhani mkuu, na makuhani wa daraja ya pili, na walinzi wa mlango, kwamba watoe katika hekalu la Bwana vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali, na kwa ajili ya Ashera, na kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni; akavipiga moto nje ya Yerusalemu, katika mashamba ya Ridroni, akayachukua majivu yake mpaka Betheli.

5Akawaondosha wale makuhuni walioabudu sanamu, ambao wafalme wa Yuda waliwaweka ili kufukiza uvumba katika mahali pa juu, ndani ya miji ya Yuda, na katika kila mahali, pande zote za Yerusalemu; na hao pia waliomfukizia uvumba Baali, na jua, na mwezi, na sayari, na jeshi lote la mbinguni.

6Naye akaiondoa Ashera katika nyumba ya Bwana, nje ya Yerusalemu, mpaka Kidroni, akaipiga moto penye kijito cha Kidroni, na kuiponda-ponda iwe mavumbi, akayatupa mavumbi yake juu ya makaburi ya watu.

7Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa Bwana, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera.

8Akawatoa makuhani wote katika miji ya Yuda, akapanajisi mahali pa juu, makuhani walipokuwa wamefukiza uvumba, tangu Geba hata Beer-sheba; akapavunja mahali pa juu pa malango, palipokuwapo penye kuingia lango la Yoshua, liwali wa mji, palipokuwa upande wa kushoto wa mtu langoni pa mji.

9Walakini hao makuhani wa mahali pa juu hawakupanda madhabahuni kwa Bwana katika Yerusalemu, bali wakala mikate isiyo na chachu katikati ya ndugu zao.

10Naye akainajisi Tofethi, iliyomo katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu asipitishe mwana wake au binti yake motoni kwa Moleki.

11Akawaondoa farasi ambao wafalme wa Yuda waliwatoa kwa jua, hapo pa kuingia nyumbani mwa Bwana, karibu na chumba cha Nathan-Meleki, towashi, kilichohuwako kiungani; akayapiga moto magari ya jua.

12Nazo madhabahu zilizokuwako darini juu ya chumba cha juu cha Ahazi, wafalme wa Yuda walizozifanya, nazo madhabahu alizozifanya Manase katika behewa mbili za nyumba ya Bwana, mfalme akazivunja, akazitelemsha huko nje, na kuyatupa mavumbi yake katika kijito cha Kidroni.

13Na mahali pa juu palipokuwapo mbele ya Yerusalemu, palipokuwa upande wa kuume wa mlima wa uharibifu, alipopajenga Sulemani, mfalme wa Israeli, kwa Ashtorethi, chukizo la Wasidoni, na Kemoshi, chukizo la Moabu, na Milkomu, chukizo la wana wa Amoni, mfalme akapanajisi.

14Akazivunja-vunja nguzo, akayakata-kata maashera, akapajaza mahali pake mifupa ya watu.

15Tena zaidi ya hayo, ile madhabahu iliyokuwako Betheli, na mahali pa juu alipopafanya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli, madhabahu hiyo aliibomoa; na mahali pa juu alipateketeza, akapaponda-ponda hata pakawa mavumbi, akaiteketeza ile Ashera.

16Naye Yosia alipogeuka, aliyaona makaburi yale yaliyokuwako huko, juu ya mlima; akatuma watu, akaitoa ile mifupa katika yale makaburi, akaiteketeza juu ya madhabahu, akainajisi, sawasawa na lile neno la Bwana, alilolinena yule mtu wa Mungu, aliyetamka mambo hayo.

17Kisha akasema, Ni kumbukumbu la nani, hili ninaloliona? Na watu wa mji wakamwambia, Ni kaburi la yule mtu wa Mungu, aliyetoka Yuda, akayanena mambo hayo uliyoyatenda wewe juu ya madhabahu ya Betheli.

18Akasema, Mwacheni; mtu awaye yote asiiondoe mifupa yake. Basi wakaiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya yule nabii aliyetoka Samaria.

19Na nyumba zote pia za mahali pa juu palipokuwa katika miji ya Samaria, wafalme wa Israeli walizozifanya, ili kumkasirisha Bwana, Yosia aliziondoa, akazitenda kwa mfano wa mambo yote aliyoyatenda katika Betheli.

20Akawaua na makuhani wote wa mahali pa juu waliokuwako huko, juu ya madhabahu, akateketeza mifupa ya watu juu yake; kisha akarejea Yerusalemu.

21Naye mfalme akawaamuru watu wote, akasema, Mfanyieni Bwana, Mungu wenu, pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano.

22Hakika yake haikufanyika pasaka kama hiyo, tangu zamani za waamuzi waliowaamua Israeli, wala katika zamani za wafalme wa Israeli, wala za wafalme wa Yuda.

23Bali katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia ilifanyika pasaka hii kwa Bwana ndani ya Yerusalemu.

24Tena wenye pepo wa utambuzi, na wachawi, na vinyago, na sanamu, na machukizo yote yaliyoonekana katika nchi ya Yuda na katika Yerusalemu, Yosia akayaondoa yote, ili apate kuyathibitisha maneno ya torati yaliyoandikwa katika kile kitabu alichokiona Hilkia kuhani ndani ya nyumba ya Bwana.

25Kabla ya huyo hapakuwa na mfalme mfano wake, aliyemwelekea Bwana kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na sheria zote za Musa; wala baada yake hakuinuka mmoja mfano wake yeye.

26Walakini Bwana hakuuacha ukali wa ghadhabu yake nyingi, ambayo kwayo hasira yake iliwaka juu ya Yuda, kwa sababu ya machukizo yote ambayo Manase amemchukiza.

27Bwana akasema Nitawahamisha Yuda pia mbali nami, kama nilivyowahamisha Israeli, nami nitautupa mji huu niliouchagua, naam, Yerusalemu, na nyumba ile niliyoinena, Jina langu litakuwa humo.

28Basi mambo yote ya Yosia yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?

29Katika siku zake, Farao-neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana na mfalme wa Ashuru, akafika mto Frati; naye mfalme Yosia akaenda kupigana naye; naye mfalme wa Misri akamwua huko Megido, hapo alipoonana naye.

30Watumishi wake wakamchukua garini, amekwisha kufa, kutoka Megido, wakamleta Yerusalemu, wakamzika katika kaburi lake mwenyewe. Watu wa nchi wakamtwaa Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtia mafuta, wakamtawaza awe mfalme badala ya baba yake.

31Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali binti Yeremia wa Libna.

32Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake.

33Naye Farao-neko akamfunga huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, ili asitawale huko Yerusalemu. Akaitoza nchi kodi talanta mia za fedha na talanta ya dhahabu.

34Farao-neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia awe mfalme mahali pa Yosia babaye, akambadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu, lakini akamwondoa Yehoahazi; akaenda naye Misri, naye akafa huko.

35Na Yehoyakimu akampa Farao dhahabu na fedha; lakini akaitoza nchi kodi, ili apate kutoa zile fedha kwa amri yake Farao; akawatoza fedha na dhahabu watu wa nchi, kila mtu kwa kodi yake, ili ampe Farao-neko.

36Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Zebida binti Pedaya wa Ruma.

37Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake.