2 Samweli - Sura ya 11

2 Samweli - Sura ya 11

1Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu.

2Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho.

3Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti?

4Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake.

5Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito.

6Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, Unipelekee Uria, Mhiti. Naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi.

7Uria alipomwendea Daudi, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, na habari za watu, na habari za vita.

8Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme.

9Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake.

10Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake, Daudi akamwambia Uria, Je! Hukutoka safarini? Mbona hukushuka nyumbani kwako?

11Naye Uria akamwambia Daudi, Sanduku, na Israeli, na Yuda, wanakaa vibandani; na bwana wangu Yoabu, na watumishi wa bwana wangu, wamepiga kambi waziwazi uwandani; nami niende nyumbani kwangu, kula na kunywa, na kulala na mke wangu? Uishivyo, na kama roho yako iishivyo, mimi sitafanya jambo hili.

12Basi Daudi akamwambia Uria, Ngoja hapa leo tena, na kesho nitakuacha kwenda zako. Basi Uria akakaa Yerusalemu siku ile, na siku ya pili yake.

13Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hata wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake.

14Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria.

15Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe.

16Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa.

17Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa.

18Ndipo Yoabu akapeleka na kumwarifu Daudi habari zote za vita;

19akamwagiza yule mjumbe, akisema, Ukiisha kumpa mfalme habari zote za vita,

20itakuwa, hasira ya mfalme ikiwaka, akakuambia, Kwani mliukaribia mji namna ile ili kuupiga? Je! Hamkujua ya kuwa watapiga mishale toka ukutani?

21Ni nani aliyempiga Ahimeleki, mwana wa Yeru-beshethi? Je! Si mwanamke aliyemtupia jiwe la kusagia la juu kutoka ukutani? Hata akafa huko Thebesi? Kwani kuukaribia ukuta namna ile? Ndipo utakaposema, Mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa naye.

22Basi yule mjumbe akaenda, akafika na kumwonyesha Daudi yote aliyomtuma Yoabu.

23Yule mjumbe akamwambia Daudi, Watu hao walitushinda, wakatutokea nje hata uwandani, tukashindana nao hata mahali pa kuingilia langoni.

24Wapiga mishale wakatupiga sisi, watumishi wako, toka juu ya ukuta; na baadhi ya watumishi wa mfalme wamekufa, na Uria, Mhiti, mtumishi wako, amekufa naye.

25Basi Daudi akamwambia yule mjumbe, Basi, mwambie Yoabu maneno haya, Jambo hili lisiwe baya machoni pako, maana upanga hula huyu kama unavyomla huyu; zidi kutia nguvu vita vyako juu ya mji ukauangushe; nawe mtie moyo.

26Na yule mke wa Uria alipopata habari ya kuwa Uria mumewe amekufa, akamwombolezea mumewe.

27Hata maombolezo hayo yalipokwisha, Daudi akatuma mtu, akamtwaa, akamtia nyumbani mwake; naye akawa mkewe, akamzalia mwana. Lakini jambo lile alilolitenda Daudi likamchukiza Bwana.