2 Samweli - Sura ya 16

2 Samweli - Sura ya 16

1Naye Daudi alipokipita punde hicho kilele cha mlima, tazama, Siba, mtumwa wa Mefiboshethi, akamkuta, na punda wawili waliotandikwa, na juu yao mikate mia mbili ya ngano, na vishada mia vya zabibu kavu, na matunda mia ya wakati wa hari, na kiriba cha divai.

2Mfalme akamwambia Siba, Ni za nini hizi? Siba akasema, Punda ni za jamaa ya mfalme wazipande; na mkate na matunda ni chakula cha hawa vijana; na divai ni kwamba wanywe hao wazimiao nyikani.

3Mfalme akasema, Na mwana wa bwana wako yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Angalia, anakaa Yerusalemu; kwani alisema, Leo nyumba ya Israeli watanirudishia ufalme wa baba yangu.

4Ndipo mfalme akamwambia Siba, Tazama, yote yaliyokuwa ni mali ya Mefiboshethi ni yako. Siba akasema, Mimi nasujudu; na nione kibali machoni pako, Ee bwana wangu, mfalme.

5Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda.

6Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto.

7Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa!

8Bwana amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye Bwana ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu.

9Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake.

10Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu Bwana amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya?

11Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza.

12Labda Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo.

13Basi wakaendelea njiani Daudi na watu wake; Shimei naye akaaendelea juu ya ubavu wa kile kilima, kwa kumkabili, huku akiendelea, akilaani, akimtupia mawe, na kurusha mavumbi.

14Naye mfalme na watu wake wote waliokuwa pamoja naye wakafika, wamechoka sana; naye akajiburudisha huko.

15Absalomu, na hao watu wote wa Israeli, wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye.

16Ikawa, Hushai, Mwarki, rafiki wa Daudi, alipomjia Absalomu, Hushai akamwambia Absalomu, Na aishi mfalme, aishi mfalme.

17Naye Absalomu akamwambia Hushai, Je! Huu ndio wema wako kwa rafiki yako? Mbona hukutoka pamoja na rafiki yako?

18Hushai akamwambia Absalomu, La, sivyo; lakini yule Bwana aliyemchagua, na watu hawa, na watu wote wa Israeli, mimi nitakuwa wake, na pamoja naye nitakaa.

19Na tena, Ni nani ambaye yanipasa nimtumikie? Hainipasi kutumika mbele ya mwanawe? Kama nilivyotumika mbele ya baba yako, ndivyo nitakavyokuwa mbele yako.

20Kisha Absalomu akamwambia Ahithofeli, Haya, toa shauri lako, tufanyeje.

21Naye Ahithofeli akamwambia Absalomu, Ingia wewe kwa masuria ya baba yako, hao aliowaacha ili kutunza nyumba; na Israeli wote watasikia ya kuwa umechukizwa kabisa na baba yako; ndipo itatiwa nguvu mikono yao wote walio pamoja nawe.

22Basi wakamtandikia Absalomu hema juu ya nyumba darini; naye Absalomu akaingia kwa masuria ya babaye machoni pa Israeli wote.

23Na shauri lake Ahithofeli, alilokuwa akilitoa siku zile, lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu; ndivyo yalivyokuwa mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa Absalomu.