2 Samweli - Sura ya 17

2 Samweli - Sura ya 17

1Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu;

2nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake;

3na hao watu wote nitawarejeza kwako; mtu yule umtafutaye ni kana kwamba wamerudi wote; na hivyo watu wote watakuwa katika amani.

4Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli.

5Ndipo Absalomu akasema, Basi, mwiteni Hushai, Mwarki, naye, tukasikie atakayosema yeye pia.

6Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako.

7Hushai akamwambia Absalomu, Shauri hili alilolitoa Ahithofeli si jema wakati huu.

8Hushai akafuliza kusema, Wamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake.

9Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna machinjo katika watu wanaofuatana na Absalomu.

10Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa.

11Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe.

12Hivyo tutamfikia mahali po pote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye.

13Tena, ikiwa amejitia katika mji uwao wote, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake.

14Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema kuliko shauri la Ahithofeli. Kwa maana Bwana alikuwa amekusudia kulivunja shauri jema la Ahithofeli, ili Bwana alete mabaya juu ya Absalomu.

15Ndipo Hushai akawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani, Ahithofeli amempa Absalomu na wazee wa Israeli mashauri kadha wa kadha; na mimi nimetoa mashauri kadha wa kadha.

16Basi sasa pelekeni habari upesi kamwambieni Daudi ya kwamba, Usilale usiku huu karibu na vivuko vya jangwani; bali usikose kuvuka; asije akamezwa mfalme, na watu wote walio pamoja naye.

17Basi Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakikaa karibu na Enrogeli; na mjakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapa habari; nao huenda kumwambia mfalme Daudi; maana ilikuwa lazima wasionekane wakiingia mjini.

18Lakini kijana mmoja aliwaona, akamwambia Absalomu; basi wakaenda wote wawili kwa haraka, wakafika Bahurimu, nyumbani kwa mtu aliyekuwa na kisima uani mwake; wakashuka ndani yake.

19Na mwanamke akatwaa kifuniko akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima, akaanika ngano iliyotwangwa juu yake; wala halikujulikana neno lo lote.

20Nao watumishi wa Absalomu wakamwendea yule mwanamke mle nyumbani; wakasema, Wako wapi Yonathani na Ahimaasi? Yule mwanamke akawaambia, Wamevuka kijito cha maji. Basi walipokwisha kuwatafuta wasiwaone, wakarudi Yerusalemu.

21Kisha ikawa, baada ya kuondoka kwao, wale wakatoka kisimani, wakaenda wakamwarifu mfalme Daudi; wakamwambia Daudi, Ondokeni, mkavuke maji haya upesi; maana ndivyo alivyotoa shauri Ahithofeli juu yenu.

22Ndipo Daudi, na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakaondoka, wakavuka Yordani; na kulipopambazuka hakubaki mmojawapo wao asiyevuka Yordani.

23Naye Ahithofeli alipoona ya kuwa shauri lake halikufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka, akaenda nyumbani kwake, mjini mwake, akaitengeneza nyumba yake, akajisonga; akafa, akazikwa kaburini mwa babaye.

24Basi Daudi akaja Mahanaimu. Naye Absalomu akauvuka Yordani yeye na watu wote wa Israeli pamoja naye.

25Naye Absalomu akamweka Amasa awe juu ya jeshi mahali pa Yoabu. Basi huyo Amasa alikuwa mwana wa mtu, jina lake Yetheri, Mwishmaeli, aliyeingia kwa Abigali, binti Nahashi, nduguye Seruya, mamaye Yoabu.

26Israeli na Absalomu wakapiga kambi katika nchi ya Gileadi.

27Ikawa, Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi, mwana wa Nahashi wa Raba, wa wana wa Amoni, na Makiri, mwana wa Amieli wa Lo-debari, na Barzilai, Mgileadi wa Rogelimu,

28wakaleta magodoro, na mabakuli, na vyungu, na ngano, na shayiri, na unga, na bisi, na kunde, na dengu,

29na asali, na siagi, na kondoo, na samli ya ng'ombe, wapate kula Daudi na watu waliokuwa pamoja naye; kwani walisema, Watu hao waona njaa, tena wamechoka, nao wana kiu huku nyikani.