2 Samweli - Sura ya 4

2 Samweli - Sura ya 4

1Hata Ishboshethi mwana wa Sauli aliposikia ya kuwa Abneri amekufa huko Hebroni, mikono yake ilikuwa dhaifu, na Waisraeli wote wakataabika.

2Na huyo mwana wa Sauli alikuwa na watu wawili, maakida wa vikosi; jina lake mmoja akiitwa Baana, na jina la wa pili Rekabu wana wa Rimoni, Mbeerothi, wa wana wa Benyamini; (kwa maana Beerothi umehesabiwa kuwa wa Benyamini;

3na hao Wabeerothi walikimbia kwenda Githaimu, ndipo wanapokaa hali ya ugeni hata hivi leo.)

4Naye Yonathani, mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa na kilema cha miguu. Alikuwa amepata miaka mitano, habari za Sauli na Yonathani zilipofika Yezreeli, na yaya wake akamchukua akakimbia ikawa, alipokimbia kwa haraka, huyo mtoto akaanguka, akawa kilema. Na jina lake aliitwa Mefiboshethi.

5Na wale wana wa Rimoni, Mbeerothi, Rekabu na Baana, wakaenda wakafika nyumbani kwa Ishboshethi, wakati wa hari ya mchana, alipokuwa akipumzika adhuhuri.

6Wakafikia kati ya nyumba, kana kwamba wanataka kuchukua ngano, wakampiga mkuki wa tumbo; kisha Rekabu na Baana nduguye wakakimbia.

7Basi walipoingia katika ile nyumba, alipokuwa amelala kitandani mwake, katika chumba chake cha kulala, wakampiga, wakamwua, wakamkata kichwa, wakachukua kichwa chake, wakaenda zao kwa njia ya Araba usiku kucha.

8Wakamletea Daudi kichwa cha Ishboshethi huko Hebroni, wakamwambia mfalme, Tazama, hiki ni kichwa cha Ishboshethi, mwana wa Sauli, adui yako, aliyekutafuta roho yako; Bwana amemlipia kisasi bwana wangu mfalme hivi leo, juu ya Sauli, na juu ya wazao wake.

9Naye Daudi akawajibu Rekabu na Baana, nduguye, wana wa Rimoni, Mbeerothi, akawaambia, Aishivyo Bwana, aliyenihifadhi roho yangu katika shida zote,

10mtu mmoja aliponiambia, akasema, Tazama, Sauli amekufa, akidhani ya kuwa ameleta habari njema, nalimshika, nikamwua, huko Siklagi, ndio ujira niliompa kwa habari zake.

11Basi, iwapo watu waovu wamemwua mtu mwenye haki kitandani mwake, je! Sasa nisitake zaidi damu yake mikononi mwenu, na kuwaondoa ninyi katika nchi?

12Ndipo Daudi akawaagiza vijana wake, wakawaua, wakawakata mikono na miguu, wakawatundika kando ya ziwa katika Hebroni. Nao wakakitwaa kichwa cha Ishboshethi wakakizika katika kaburi la Abneri huko Hebroni.