2 Timotheo - Sura ya 2

2 Timotheo - Sura ya 2

1Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu.

2Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.

3Ushiriki taabu pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu.

4Hakuna apigaye vita ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari.

5Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali.

6Yampasa mkulima mwenye taabu ya kazi kuwa wa kwanza wa kupata fungu la matunda.

7Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote.

8Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu.

9Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi.

10Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.

11Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia;

12Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi;

13Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.

14Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao.

15Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.

16Jiepushe na maneno yasiyo na maana, ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu,

17na neno lao litaenea kama donda-ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto,

18walioikosa ile kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha kuwapo, hata kuipindua imani ya watu kadha wa kadha.

19Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake.

20Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina.

21Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema.

22Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.

23Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi.

24Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;

25akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;

26wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.