Matendo ya Mitume - Sura ya 22

Matendo ya Mitume - Sura ya 22

1Enyi wanaume, ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni, nikijitetea mbele yenu sasa.

2Waliposikia kwamba anasema nao kwa lugha ya Kiebrania wakazidi kunyamaza; akasema,

3Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi;

4nikawaudhi watu wa Njia hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake.

5Kama Kuhani Mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe.

6Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote.

7Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi?

8Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi.

9Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami.

10Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye.

11Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski.

12Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko,

13Akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile.

14Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake.

15Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia.

16Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.

17Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa hali ya kuzimia roho,

18nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu.

19Nami nikasema, Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nalikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi.

20Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua.

21Naye akaniambia, Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa.

22Wakamsikiliza mpaka neno lile, wakapaza sauti zao, wakisema, Mwondoe huyu katika nchi, kwa maana haifai aishi.

23Walipokuwa wakipiga kelele na kutupa mavazi yao na kurusha-rusha mavumbi juu,

24yule jemadari akaamuru aletwe ndani ya ngome, akisema aulizwe habari zake kwa kupigwa mijeledi, ili ajue sababu hata wakampigia kelele namna hii.

25Hata walipokwisha kumfunga kwa kamba, Paulo akamwambia yule akida aliyesimama karibu, Je! Ni halali ninyi kumpiga mtu aliye Mrumi naye hajakuhumiwa bado?

26Yule akida aliposikia, akaenda akamwarifu yule jemadari, akisema, Unataka kufanya nini? Kwa maana mtu huyu ni Mrumi.

27Jemadari akaja, akamwuliza, Niambie, u Mrumi? Akasema, Ndiyo.

28Jemadari akajibu, Mimi nalipata wenyeji huu kwa mali nyingi. Paulo akasema, Na mimi ni Mrumi wa kuzaliwa.

29Basi wale waliokuwa tayari kumwuliza wakaondoka wakamwacha. Na yule jemadari naye akaogopa, alipojua ya kuwa ni Mrumi, na kwa sababu amemfunga.

30Siku ya pili yake akitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao.