Matendo ya Mitume - Sura ya 27

Matendo ya Mitume - Sura ya 27

1Basi ilipoamriwa tuabiri hata Italia, wakamtia Paulo na wafungwa wengine katika mikono ya akida mmoja, jina lake Yulio, wa kikosi cha Augusto.

2Tukapanda katika merikebu ya Adramitio iliyokuwa tayari kusafiri mpaka miji ya pwani za Asia, tukatweka; Aristarko, Mmakedonia wa Thesalonike, akiwa pamoja nasi.

3Siku ya pili tukawasili Sidoni; Yulio akamfadhili sana Paulo akampa ruhusa kwenda kwa rafiki zake, apate kutunzwa.

4Kutoka huko tukatweka, tukasafiri chini ya Kipro ili kuukinga upepo, kwa maana pepo zilikuwa za mbisho.

5Tulipopita bahari ya upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira, mji wa Likia.

6Na huko yule akida akakuta merikebu ya Iskanderia, tayari kusafiri kwenda Italia, akatupandisha humo.

7Tukasafiri polepole kwa muda wa siku nyingi, tukafika mpaka Nido kwa shida; na kwa sababu upepo ulikuwa ukituzuia tukapita chini ya Krete, tukaikabili Salmone.

8Tukaipita kwa shida, pwani kwa pwani, tukafika mahali paitwapo Bandari Nzuri. Karibu na hapo pana mji uitwao Lasea.

9Na wakati mwingi ulipokwisha kupita, na safari ikiwa ina hatari sasa, kwa sababu siku za kufunga zilikuwa zimekwisha kupita, Paulo akawaonya,

10akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na ya maisha yetu pia.

11Lakini yule akida akawasikiliza nahodha na mwenye merikebu zaidi ya yale aliyoyasema Paulo.

12Na kwa sababu bandari ile ilikuwa haifai kukaa wakati wa baridi, wengi wao wakatoa shauri la kutweka kutoka huko ili wapate kufika Foinike, kama ikiwezekana, na kukaa huko wakati wa baridi; nayo ni bandari ya Krete, inaelekea kaskazini-mashariki na kusini-mashariki.

13Na upepo wa kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu kupata, wakang'oa nanga, wakasafiri karibu na Krete pwani kwa pwani.

14Baada ya muda mchache ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo,

15merikebu iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa.

16Na tukipita upesi karibu na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza mashua; lakini kwa shida.

17Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza merikebu kwa kupitisha kamba chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika fungu liitwalo Sirti, wakatua matanga wakachukuliwa vivi hivi.

18Na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, siku ya pili yake wakaanza kuitupa shehena baharini.

19Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe.

20Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka.

21Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii.

22Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu.

23Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami,

24akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe.

25Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.

26Lakini hatuna budi kupwelewa katika kisiwa kimoja.

27Hata usiku wa kumi na nne ulipofika, tulipokuwa tukichukuliwa huko na huko katika bahari ya Adria, kama usiku wa manane baharia wakadhani ya kuwa wanaikaribia nchi kavu.

28Wakatupa bildi wakapata pima ishirini, wakaendelea kidogo wakatupa bildi tena, wakapata pima kumi na tano.

29Wakachelea tusije tukapwelewa mahali penye miamba, wakatupa nanga nne za tezi, wakaomba kuche.

30Na baharia walipotaka kukimbia na kuiacha merikebu, wakiishusha mashua baharini kana kwamba wanataka kutupa nanga za omo,

31Paulo akawaambia akida na askari, Hawa wasipokaa ndani ya merikebu hamtaweza kuokoka.

32Basi askari wakazikata kamba za mashua, wakaiacha ianguke.

33Na kulipokuwa kukipambauka Paulo akawasihi wote wale chakula, akisema, Leo ni siku ya kumi na nne kungoja na kufunga, hamkula kitu cho chote.

34Basi nawasihi mle chakula, maana itakuwa kwa wokovu wenu; kwa maana hapana hata unywele wa kichwa cha mmoja wenu utakaopotea.

35Alipokwisha kusema hayo akatwaa mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote akaumega akaanza kula.

36Ndipo wakachangamka wote, wakala chakula wenyewe.

37Na sisi tuliokuwa ndani ya merikebu tulipata watu mia mbili na sabini na sita.

38Walipokwisha kushiba wakaipunguza shehena ya merikebu, wakiitupa ngano baharini.

39Kulipokucha hawakuitambua ile nchi, ila waliona hori yenye ufuo, wakashauriana kuiegesha merikebu huko, kama ikiwezekana.

40Wakazitupilia mbali zile nanga, na kuziacha baharini, pamoja na kuzilegeza kamba za sukani, wakalitweka tanga dogo ili liushike upepo, wakauendea ule ufuo.

41Lakini wakafikia mahali palipokutana bahari mbili, wakaiegesha merikebu, omo ikakwama ikakaa isitikiswe, bali tezi ilikuwa imefumuliwa kwa nguvu za mawimbi.

42Shauri la askari lilikuwa kuwaua wafungwa, mtu asiogelee na kukimbia.

43Bali akida, akitaka kumponya Paulo, akawazuia, wasifanye kama walivyokusudia, akawaamuru wale wawezao kuogelea wajitupe kwanza baharini, wafike nchi kavu;

44nao waliosalia, hawa juu ya mbao na hawa juu ya vitu vingine vya merikebu. Na hivyo watu wote wakapata kuifikilia nchi kavu salama.