Matendo ya Mitume - Sura ya 7

Matendo ya Mitume - Sura ya 7

1Kuhani Mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo?

2Naye akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Ibrahimu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani,

3akamwambia, Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi nitakayokuonyesha.

4Ndipo alipotoka katika nchi ya Wakaldayo, akakaa Harani, akatoka huko baada ya kufa babaye, Mungu akamhamisha mpaka nchi hii mnayokaa ninyi sasa.

5Wala hakumpa urithi humu hata kiasi cha kuweka mguu; akaahidi kwamba atampa, iwe milki yake, na ya uzao wake baadaye alipokuwa hana mtoto.

6Mungu akanena hivi, ya kwamba wazao wake watakuwa wageni katika nchi ya watu wengine, nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka mia nne.

7Na lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa.

8Akampa agano la tohara; basi Ibrahimu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu.

9Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja naye,

10akamtoa katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote.

11Basi kukawa njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, na dhiki nyingi, wala baba zetu hawakupata chakula cha kuwatosha.

12Hata Yakobo aliposikia ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu mara ya kwanza.

13Hata safari ya pili Yusufu akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusufu ikawa dhahiri kwa Farao.

14Yusufu akatuma watu akamwita Yakobo babaye na jamaa zake wote pia, watu sabini na watano.

15Basi Yakobo akashuka mpaka Misri; akafa yeye na baba zetu;

16wakachukuliwa mpaka Shekemu wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Ibrahimu alilinunua kwa kima cha fedha kwa wana wa Hamori, huko Shekemu.

17Basi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri,

18hata mfalme mwingine akainuka juu ya Misri, asiyemfahamu Yusufu.

19Huyo akawafanyia hila kabila yetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru wawatupe watoto wao wachanga, ili wasiishi.

20Wakati huo akazaliwa Musa, naye alikuwa mzuri sana, akalelewa muda wa miezi mitatu katika nyumba ya babaye.

21Hata alipotupwa, binti Farao akamtwaa, akamlea awe kama mwanawe.

22Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo.

23Umri wake ulipopata kama miaka arobaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli.

24Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri.

25Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu.

26Siku ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana?

27Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu?

28Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana?

29Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Midiani, akazaa wana wawili huko.

30Hata miaka arobaini ilipotimia, malaika wa Bwana akamtokea katika jangwa la mlima wa Sinai katika mwali wa moto, kijitini.

31Musa alipouona, akastaajabia maono yale, na alipokaribia ili atazame, sauti ya Bwana ikamjia,

32Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akatetemeka, asithubutu kutazama.

33Bwana akamwambia, Vua viatu miguuni mwako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni nchi takatifu.

34Yakini nimeona mateso ya watu wangu waliomo Misri, nimesikia kuugua kwao, nami nimeshuka niwatoe. Basi sasa, nitakutuma mpaka Misri.

35Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kijiti.

36Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arobaini.

37Musa huyo ndiye aliyewaambia Waisraeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye.

38Yeye ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani pamoja na yule malaika aliyesema naye katika mlima wa Sinai, tena pamoja na baba zetu; ndiye aliyepokea maneno ya uzima atupe sisi.

39Mtu huyo baba zetu hawakutaka kumtii, bali wakamsukumia mbali, na kwa mioyo yao wakarejea Misri,

40wakamwambia Haruni, Tufanyie miungu, watakaotutangulia; maana huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui lililompata.

41Wakafanya ndama siku zile, wakaleta dhabihu kwa sanamu ile, wakafurahia kazi za mikono yao.

42Basi Mungu akaghairi, akawaacha ili waliabudu jeshi la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika chuo cha manabii, Je! Mlinitolea mimi dhabihu na sadaka Miaka arobaini katika jangwa, enyi nyumba ya Israeli?

43Nanyi mlichukua hema ya Moleki, Na nyota za mungu wenu Refani, Sanamu mlizozifanya ili kuziabudu; Nami nitawafahamisha mwende mbali kupita Babeli.

44Ile hema ya ushahidi ilikuwa pamoja na baba zetu jangwani, kama alivyoagiza yeye aliyesema na Musa, ya kwamba aifanye sawasawa na mfano ule aliouona;

45ambayo baba zetu, kwa kupokezana, wakaiingiza pamoja na Yoshua katika milki ya Mataifa wale, ambao Mungu aliwafukuza mbele ya baba zetu, mpaka siku za Daudi;

46aliyepata fadhili mbele za Mungu, naye aliomba ampatie Mungu wa Yakobo maskani.

47Lakini Sulemani alimjengea nyumba.

48Ila Yeye aliye juu hakai katika nyumba zilizofanywa kwa mikono, kama vile asemavyo nabii,

49Mbingu ni kiti changu cha enzi, Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu; Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema Bwana,

50Au ni mahali gani nitakapostarehe? Si mkono wangu uliofanya haya yote?

51Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.

52Ni yupi katika manabii ambaye baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa mmekuwa wasaliti wake, mkamwua;

53ninyi mlioipokea torati kwa agizo la malaika msiishike.

54Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno.

55Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu.

56Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.

57Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,

58wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.

59Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu.

60Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.