Matendo ya Mitume - Sura ya 8

Matendo ya Mitume - Sura ya 8

1Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume.

2Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu.

3Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani.

4Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno.

5Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo.

6Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya.

7Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa.

8Ikawa furaha kubwa katika mji ule.

9Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa.

10Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu.

11Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake.

12Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.

13Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka.

14Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana;

15ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu;

16kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu.

17Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.

18Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema,

19Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu.

20Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.

21Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.

22Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako.

23Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu.

24Simoni akajibu, akasema, Niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikilie mambo haya mliyosema hata moja.

25Nao walipokwisha kushuhudia na kulihubiri neno la Bwana wakarudi Yerusalemu, wakaihubiri Injili katika vijiji vingi vya Wasamaria.

26Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa.

27Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu,

28akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya.

29Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.

30Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?

31Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.

32Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake.

33Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.

34Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?

35Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.

36Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?

37Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]

38Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza.

39Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.

40Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria.