Amosi - Sura ya 1

1Maneno ya Amosi, aliyekuwa mmoja wa wachungaji wa Tekoa; maono aliyoyaona katika habari za Israeli, siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli, miaka miwili kabla ya tetemeko la nchi.
2Naye alisema, Bwana atanguruma toka Sayuni, Atatoa sauti yake toka Yerusalemu; Na malisho ya wachungaji yataomboleza, Na kilele cha Karmeli kitanyauka.
3Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Dameski, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameipura Gileadi kwa vyombo vya kupuria vya chuma;
4lakini nitapeleka moto uingie katika nyumba ya Hazaeli, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi.
5Nami nitalivunja komeo la Dameski, na kuwakatilia mbali wenyeji wa bondeni mwa Aveni, na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Beth-Adini; na watu wa Shamu watakwenda hali ya kufungwa hata Kiri, asema Bwana.
6Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Gaza, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu waliichukua katika hali ya kufungwa kabila nzima, wawatie katika mikono ya Edomu;
7lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Gaza, nao utayateketeza majumba yake.
8Nami nitamkatilia mbali mwenyeji katika Ashdodi; na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Ashkeloni; nami nitaugeuza mkono wangu uwe juu ya Ekroni; na mabaki ya Wafilisti wataangamia, asema Bwana MUNGU.
9Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Tiro, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameitia kabila nzima katika mikono ya Edomu, wala hawakulikumbuka agano la udugu;
10lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Tiro, nao utayateketeza majumba yake.
11Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Edomu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga, akatupilia mbali huruma zake zote; hasira yake ikararua-rarua daima, akaishika ghadhabu yake milele;
12lakini nitapeleka moto juu ya Temani, nao utayateketeza majumba ya Bosra.
13Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya wana wa Amoni, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewapasua wanawake wa Gileadi wenye mimba, ili wapate kuongeza mipaka yao;
14lakini nitawasha moto katika ukuta wa Raba, nao utayateketeza majumba yake; pamoja na kupiga kelele siku ya vita, pamoja na tufani katika siku ya chamchela;
15na mfalme wao atakwenda utumwani, yeye na wakuu wake wote pamoja, asema Bwana.