Amosi - Sura ya 9

Amosi - Sura ya 9

1Nalimwona Bwana akisimama karibu na madhabahu; akasema, vipigo vichwa vya nguzo, hata vizingiti vitikisike; vivunje vipande vipande juu ya kichwa cha kila mmoja wao; nami nitamwua mtu wa mwisho wao kwa upanga; hapana hata mmoja wao atakayekimbia, wala hataokoka hata mmoja wao.

2Wajapochimba waingie katika kuzimu, mkono wangu utawatoa huko; nao wajapopanda hata mbinguni, nitawatelemsha toka huko.

3Nao wajapojificha katika kilele cha Karmeli, nitawatafuta na kuwatoa toka huko; na wajapositirika katika vilindi vya bahari nisiwaone, nitamwagiza joka huko, naye atawauma.

4Nao wajapokwenda hali ya kufungwa mbele ya adui zao, nitauagiza upanga huko, nao utawaua; nami nitawaelekezea macho yangu niwatende mabaya, wala si mema.

5Kwa maana Bwana, MUNGU wa majeshi, ndiye aigusaye nchi, nayo ikayeyuka, na wote wakaao ndani yake wataomboleza; nayo itainuka yote pia kama Mto, nayo itakupwa tena kama Mto wa Misri.

6Yeye ndiye avijengaye vyumba vyake mbinguni, na kuweka misingi ya kuba yake juu ya nchi; yeye ndiye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; Bwana ndilo jina lake.

7Je! Ninyi si kama wana wa Wakushi kwangu mimi, enyi wana wa Israeli, asema Bwana? Je! Mimi sikuwapandisha Israeli toka nchi ya Misri, na Wafilisti toka Kaftori, na Washami toka Kiri?

8Angalieni, macho ya Bwana MUNGU yanauangalia ufalme wenye dhambi, nami nitauangamiza utoke juu ya uso wa dunia; lakini sitaiangamiza kabisa nyumba ya Yakobo, asema Bwana.

9Kwa maana, angalieni, nitatoa amri, nami nitaipepeta nyumba ya Israeli katika mataifa yote, kama vile ngano ipepetwavyo katika ungo lakini hata chembe moja iliyo ndogo haitaanguka chini.

10Wenye dhambi wote katika watu wangu watakufa kwa upanga, hao wasemao, Mabaya hayatatupata nyuma wala mbele.

11Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale;

12wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema Bwana, afanyaye hayo.

13Angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo huyo alimaye atamfikilia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka.

14Nami nitawarejeza tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watafanyiza bustani, na kula matunda yake.

15Nami nitawapanda katika nchi yao, wala hawatang'olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa, asema Bwana, Mungu wako.