Wakolosai - Sura ya 2

Wakolosai - Sura ya 2

1Maana nataka ninyi mjue jinsi ilivyo kuu juhudi yangu niliyo nayo kwa ajili yenu, na kwa ajili ya wale wa Laodikia, na wale wasioniona uso wangu katika mwili;

2ili wafarijiwe mioyo yao, wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo;

3ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika.

4Nasema neno hili, mtu asije akawadanganya kwa maneno ya kuwashawishi.

5Maana nijapokuwa sipo kwa mwili, lakini nipo pamoja nanyi kwa roho, nikifurahi na kuuona utaratibu wenu na uthabiti wa imani yenu katika Kristo.

6Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye;

7wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani.

8Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.

9Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.

10Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka.

11Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo.

12Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu.

13Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote;

14akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani;

15akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.

16Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato;

17mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.

18Mtu asiwanyang'anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili;

19wala hakishiki Kichwa, ambacho kwa yeye mwili wote ukiruzukiwa na kuungamanishwa kwa viungo na mishipa, hukua kwa maongeo yatokayo kwa Mungu.

20Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani,

21Msishike, msionje, msiguse;

22(mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu?

23Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili.