Danieli - Sura ya 4

1Mfalme Nebukadreza, kwa watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wanaokaa katika dunia yote; Amani iongezeke kwenu.
2Mimi nimeona vema kutangaza habari za ishara na maajabu, aliyonitendea Mungu aliye juu.
3Ishara zake ni kubwa kama nini! Na maajabu yake yana uweza kama nini! Ufalme wake ni ufalme wa milele; na mamlaka yake ni ya kizazi hata kizazi.
4Mimi, Nebukadreza, nalikuwa nikistarehe katika nyumba yangu, nikisitawi katika nyumba yangu ya enzi.
5Nikaota ndoto iliyonitia hofu; mawazo niliyokuwa nayo kitandani mwangu, na njozi za kichwa changu, zikanifadhaisha.
6Basi nikatoa amri kwamba wenye hekima wote wa Babeli, waletwe mbele yangu, ili kunijulisha tafsiri ya ndoto ile.
7Ndipo wakaingia waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu; nikawahadithia ile ndoto; wao wasiweze kunijulisha tafsiri yake.
8Bali hatimaye Danieli akaingia mbele yangu, ambaye jina lake ni Belteshaza, kwa kufuata jina la mungu wangu; tena ndani yake inakaa roho ya miungu watakatifu; nikamhadithia ile ndoto, nikisema,
9Ee Belteshaza, mkuu wa waganga, kwa sababu ninajua ya kuwa roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako, na ya kuwa hapana neno la siri likushindalo, niambie njozi za ndoto yangu niliyoiona, na tafsiri yake.
10Njozi za kichwa changu kitandani mwangu zilikuwa hivi; naliona, na tazama, palikuwa na mti katikati ya nchi, urefu wake mkubwa sana.
11Mti ule ukakua, ukawa na nguvu, urefu wake ulifika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka mwisho wa dunia.
12Majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha watu wote; wanyama wa kondeni walipata uvuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake; kila kitu chenye mwili kilipata chakula kwake.
13Nikaona katika njozi za kichwa changu kitandani mwangu, na tazama, mlinzi, naye ni mtakatifu, alishuka kutoka mbinguni.
14Akapaza sauti yake, akasema, Ukateni mti huu, yafyekeni matawi yake, yapukusieni mbali majani yake, na kuyatawanya matunda yake, wanyama na waondoke hapo chini yake, na ndege katika matawi yake.
15Walakini kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikapate maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama katika majani ya nchi;
16moyo wake ubadilike, usiwe moyo wa binadamu, na apewe moyo wa mnyama; nyakati saba zikapite juu yake.
17Hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi, na amri hii kwa neno la watakatifu; kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, tena humtawaza juu yake aliye mnyonge.
18Mimi, Nebukadreza, nimeiona ndoto hii; na wewe, Ee Belteshaza, eleza tafsiri yake, kwa maana wenye hekima wote wa ufalme wangu hawawezi kunijulisha tafsiri yake; bali wewe waweza, maana roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako.
19Ndipo Danieli, aliyeitwa jina lake Belteshaza, akashangaa kwa muda, na fikira zake zikamfadhaisha. Mfalme akajibu akasema, Ee Belteshaza, ndoto ile isikufadhaishe wala tafsiri yake. Belteshaza akajibu, akasema, Bwana wangu, ndoto hii iwapate wao wakuchukiao, na tafsiri yake iwapate adui zako.
20Ule mti uliouona, uliokua, ukawa na nguvu, urefu wake ukafika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka dunia yote;
21ambao majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha wote; ambao chini yake wanyama wa kondeni walikaa, na ndege wa angani walikuwa na makao yao katika matawi yake;
22ni wewe, Ee mfalme, uliyekua, na kupata nguvu; maana ukuu wako umekua na kufika mpaka mbinguni, na mamlaka yako yamefika mpaka mwisho wa dunia.
23Tena, kwa kuwa mfalme alimwona mlinzi, naye ni mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akisema, Ukateni mti huu, mkauangamize; ila kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikatiwe maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama wa kondeni, hata nyakati saba zipite juu yake;
24tafsiri yake ni hii, Ee mfalme, nayo ni amri yake Aliye juu, iliyomjia bwana wangu, mfalme;
25ya kuwa utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni, nawe utalazimishwa kula majani kama ng'ombe, nawe utatiwa maji kwa umande wa mbinguni, na nyakati saba zitapita juu yako; hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa yeye amtakaye, awaye yote.
26Na kwa kuwa waliamuru kukiacha kisiki cha shina lake; ufalme wako utakuwa imara kwako, baada ya wewe kujua ya kuwa mbingu ndizo zinazotawala.
27Kwa sababu hiyo, Ee mfalme, shauri langu lipate kibali kwako; ukaache dhambi zako kwa kutenda haki, ukaache maovu yako kwa kuwahurumia maskini; huenda ukapata kuzidishiwa siku zako za kukaa raha.
28Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza.
29Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli.
30Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?
31Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako.
32Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng'ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.
33Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng'ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.
34Hata mwisho wa siku hizo, mimi, Nebukadreza, nikainua macho yangu kuelekea mbingu, fahamu zangu zikanirudia; nikamhimidi Yeye aliye juu, nikamsifu na kumheshimu Yeye aishiye milele; kwa maana mamlaka yake ni mamlaka ya milele, na ufalme wake hudumu toka kizazi hata kizazi;
35na watu wote wanaokaa duniani wamehesabiwa kuwa si kitu, naye hufanya kama atakavyo, katika jeshi la mbinguni, na katika hao wanaokaa duniani; wala hapana awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, Unafanya nini wewe?
36Basi wakati uo huo fahamu zangu zikanirudia, na kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu, enzi yangu na fahari yangu zikanirudia; na mawaziri wangu, na madiwani wangu, wakaja kunitafuta; nami nikathibitika katika ufalme wangu, nikaongezewa enzi kupita kiasi.
37Basi mimi, Nebukadreza, namhimidi Mfalme wa mbinguni, namtukuza na kumheshimu; maana matendo yake yote ni kweli, na njia zake ni za adili; na wale waendao kwa kutakabari, yeye aweza kuwadhili.