Kumbukumbu la Torati - Sura ya 17

Kumbukumbu la Torati - Sura ya 17

1Usimchinjie Bwana, Mungu wako, ng'ombe wala kondoo aliye na kilema, wala neno ovu lo lote; kwa kuwa hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako.

2Ikiwa ameonekana katikati yako, ndani ya malango yako mojawapo, upewayo na Bwana, Mungu wako, mtu mume au mke afanyaye yaliyo maovu machoni pa Bwana, Mungu wako, kwa kuvunja maagano yake,

3naye amekwenda kutumikia miungu mingine na kuiabudu, au jua, au mwezi, au vilivyo katika jeshi la mbinguni vyo vyote, nisivyoagiza mimi;

4ukiambiwa hayo nawe umeyasikia, ndipo utafute kwa bidii, na tazama, ikiwa ni kweli lina hakika jambo lile, kuwa yafanywa machukizo kama hayo katika Israeli;

5ndipo umchukue nje malangoni kwako, yule mtu mume, au yule mwanamke, aliyefanya jambo lile ovu; ukawapige kwa mawe, wafe.

6Huyo atakayeuawa na auawe kwa midomo ya mashahidi wawili, au mashahidi watatu; asiuawe kwa mdomo wa shahidi mmoja.

7Mikono ya wale mashahidi na iwe juu yake kwanza kwa kumwua, kisha mikono ya watu wote. Uondoe vivyo uovu katikati yako.

8Ikiwa limezuka neno lililo zito kukupita wewe, katika maamuzi kati ya damu na damu, na kati ya daawa na daawa, na kati ya pigo na pigo, nayo yashindaniwa katika malango yako; ndipo nawe uondoke, ukwee uende mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako;

9uwaendee makuhani Walawi, na mwamuzi atakayekuwako siku hizo; uwaulize; nao watakuonyesha hukumu ya maamuzi;

10nawe fanya sawasawa na hukumu watakayokuonyesha mahali hapo atakapochagua Bwana; nawe tunza kufanya kwa mfano wa yote watakayokufunza;

11kwa mfano wa sheria watakayokufunza, na kwa mfano wa hukumu watakayokuambia, fanya vivyo; usigeuke katika hukumu watakayokuonyesha, kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto.

12Na mtu afanyaye kwa kujikinai, kwa kutomsikiza kuhani asimamaye hapo kwa kumtumikia Bwana, Mungu wako, au mwamuzi, na afe mtu huyo; nawe utauondoa uovu katika Israeli.

13Na hao watu wote watasikia na kuogopa, wasifanye tena kwa kujikinai.

14Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako ukaimiliki, na kukaa humo; nawe utakaposema, Nitaweka mfalme juu yangu mfano wa mataifa yote yaliyo kando-kando yangu;

15usiache kumweka yule atakayechaguliwa na Bwana, Mungu wako, awe mfalme juu yako; umweke mmoja katika ndugu zako awe mfalme juu yako; usimtawaze mgeni juu yako, ambaye si ndugu yako.

16Ila asifanye farasi wake kuwa wengi, wala asiwarudishe watu Misri, ili apate kufanya farasi kuwa wengi; kwa kuwa Bwana amewaambia, Tangu sasa msirudie tena njia ile.

17Wala asijizidishie wake, ili moyo wake usikengeuke; wala asifanye fedha zake na dhahabu kuwa nyingi mno.

18Tena na iwe, zamani aketipo juu ya kiti cha ufalme wake, ajiandikie nakala ya torati hii katika chuo, kufuata hicho kilicho mbele ya makuhani Walawi;

19na awe nayo, asome humo siku zote atakazoishi; ili apate kujifunza kumcha Bwana, Mungu wake, ayashike maneno yote ya torati hii na amri hizi, kwa kuyafanya;

20moyo wake usije ukainuliwa juu ya ndugu zake, wala asikengeuke katika maagizo, kwa mkono wa kuume wala wa kushoto; ili apate kuzifanya siku zake kuwa nyingi katika ufalme wake, yeye na wanawe, katikati ya Israeli.