Kumbukumbu la Torati - Sura ya 20

Kumbukumbu la Torati - Sura ya 20

1Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa Bwana Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri.

2Na iwe, msongeapo mapiganoni, kuhani na akaribie na kusema na watu,

3awaambie, Sikizeni, enyi Israeli, hivi leo mwasongea mapiganoni juu ya adui zenu mioyo yenu na isizime; msiche, wala msiteteme, wala msiingiwe na hofu kwa ajili ya wao;

4kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye awaandamaye kwenda kuwapigania juu ya adui zenu, ili kuwaokoa ninyi.

5Na maakida na waseme na watu, na kuwaambia, Ni mtu gani aliye hapa aliyejenga nyumba mpya, wala hajaiweka wakfu? Aende akarudi nyumbani kwake, asije akafa mapiganoni, ikawekwa wakfu na mtu mwingine.

6Ni mtu gani aliye hapa aliyepanda shamba la mizabibu, wala hajatumia matunda yake? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni, yakatumiwa na mtu mwingine matunda yake.

7Ni mtu gani aliye hapa aliyemposa mke wala hajaoa? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni, huyo mwanamke akaolewa na mume mwingine.

8Tena maakida na waseme zaidi na watu, wawaambie, Ni mtu gani aliye hapa tena mwenye hofu na moyo mnyonge? Aende akarudi nyumbani kwake, isije mioyo ya nduguze ikayeyuka mfano wa moyo wake.

9Itakuwa hapo watakapokwisha wale maakida kusema na watu, na waweke majemadari wa majeshi juu ya watu.

10Utakaposongea karibu ya mji kwenda kupigana juu yake, ndipo utakapowapigia ukelele wa amani.

11Itakuwa utakapokujibu kwa amani, na kukufungulia, ndipo watu wote watakaoonekana humo watakufanyia kazi ya shokoa, na kukutumikia.

12Na kwamba hautaki kufanya amani nawe, lakini utafanya vita juu yako, ndipo uuhusuru;

13na Bwana, Mungu wako, autiapo mkononi mwako, mpige kila mume aliyemo kwa makali ya upanga;

14lakini wanawake na watoto, na wanyama wa miji, na vilivyo mjini vyote, navyo ni nyara zake zote, uvitwae viwe mateka kwako; nawe utakula nyara za adui zako alizokupa Bwana, Mungu wako.

15Utaifanyia vivyo miji yote iliyo mbali sana nawe, isiyokuwa miji ya mataifa haya.

16Lakini katika miji ya mataifa haya akupayo Bwana, Mungu wako, kuwa urithi, usihifadhi kuwa hai kitu cho chote kipumzikacho;

17lakini uwaangamize kabisa, Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, kama alivyokuamuru Bwana, Mungu wako;

18wasije wakawafunza kufanya mfano wa machukizo yao yote, waliyoifanyia miungu yao; hivyo itakuwa ni makosa juu ya Bwana, Mungu wenu.

19Wewe utakapohusuru mji siku nyingi kwa kufanya vita juu yake, upate kuutwaa, usiangamize miti yake kwa kupeleka shoka juu yake, kwani utaweza kula matunda yake; wala usiiteme, kwa maana huo mti wa kondeni, je! Ni mtu, hata ukauzuie?

20Ila miti uijuayo si miti ya kuliwa iangamize, na kuitema; ukajenge maburuji juu ya mji ufanyao vita juu yako, hata uanguke.