Kumbukumbu la Torati - Sura ya 22

 Kumbukumbu la Torati - Sura ya 22

1Umwonapo ng'ombe wa nduguyo au kondoo wake akipotea, usijifiche kama usiyemwona; sharti utamrudisha kwa nduguyo.

2Na kwamba yule nduguyo hayupo karibu nawe, au ukiwa humjui, umchukue kwenu nyumbani kwako, uwe naye hata aje nduguyo kumtafuta, nawe mrudishie.

3Tena fanya vivyo kwa punda wake; tena fanya vivyo kwa mavazi yake; tena fanya vivyo kwa kila kitu kilichopotea cha nduguyo, kilichompotea ukakiona wewe; usijifiche kama usiyekiona.

4Umwonapo punda wa nduguyo, au ng'ombe wake, ameanguka kando ya njia, usijifiche kama usiyemwona; sharti umsaidie kumwinua tena.

5Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako.

6Kiota cha ndege kikitukia kuwa mbele yako njiani, katika mti wo wote, au chini, chenye makinda au mayai, naye koo ameatamia juu ya makinda, au juu ya mayai, usimtwae yule koo pamoja na makinda;

7sharti umwache yule koo aende zake, lakini makinda waweza kuyatwaa uwe nayo; ili upate kufanikiwa, ufanye siku zako kuwa nyingi.

8Utakapojenga nyumba mpya, fanya ukuta kando-kando ya dari lako, usije ukaleta damu juu ya nyumba yako, mtu akianguka huko.

9Usipande shamba lako la mizabibu aina mbili za mbegu; yasije yakaondolewa matunda yote, mbegu ulizopanda na maongeo ya mizabibu yako.

10Usilime kwa ng'ombe na punda wakikokota jembe pamoja.

11Usivae nguo iliyochanganyikana sufu na kitani pamoja.

12Ujifanyizie vishada katika pembe nne za mavazi yako ya kujifunika.

13Mtu akitwaa mke, akamwingilia na kumchukia,

14kisha akamshitaki mambo ya aibu kumzushia jina baya, akasema, Nimemtwaa mwanamke huyu, nami nilipomkaribia sikuona kwake alama za ubikira;

15ndipo babaye yule kijana na mamaye watakapotwaa alama za yule kijana za ubikira, wawatolee wazee wa mji langoni;

16na baba yake yule kijana awaambie wazee, Mwanamume huyu nilimpa binti yangu awe mkewe, naye amchukia;

17angalieni, amemwekea mambo ya aibu, asema, Sikuona kwa binti yako alama za ubikira, nazo hizi ndizo alama za binti yangu za ubikira. Na wayakunjue yale mavazi mbele ya wazee wa mji.

18Basi wazee wa mji ule na wamtwae yule mtu mume na kumrudi,

19wamtoze shekeli mia za fedha, wampe babaye yule kijana, kwa kuwa amemzulia jina baya mwanamwali wa Israeli; naye awe mkewe; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote.

20Lakini likiwa ni kweli neno hili, la kutoonekana kwake yule kijana alama za ubikira;

21na wamtoe nje yule kijana mlangoni pa nyumba ya baba yake, na waume wa mji wake wampige kwa mawe hata afe; kwa vile alivyofanya upumbavu katika Israeli, kwa kufanya ukahaba katika nyumba ya baba yake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.

22Akifumaniwa mtu mume amelala na mwanamke aliyeolewa na mume, na wafe wote wawili, mtu mume aliyelala na mwanamke, na yule mwanamke naye; ndivyo utakavyoondoa uovu katika Israeli.

23Pakiwa na kijana aliye mwanamwali ameposwa na mume, na mwanamume akimkuta mjini, akalala naye;

24watoeni nje katika lango la mji ule, mkawapige kwa mawe hata wafe; yule kijana, kwa kuwa hakupiga ukelele, naye yu ndani ya mji; na yule mume, kwa kuwa amemtweza mke wa mwenzake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.

25Lakini yule mtu mume kama akimkuta kondeni kijana aliyeposwa, naye mume akamtenza nguvu, akalala naye; yule mtu mume aliyelala naye na afe pekee;

26lakini yule kijana usimfanye neno; hana dhambi yule kijana ipasayo kuuawa, kwa kuwa ni mfano wa mtu kumwondokea mwenzake akamwua, ni vivyo lilivyo jambo hili;

27kwani alimkuta kondeni; yule kijana aliyeposwa akalia, pasiwe na mtu wa kumwokoa.

28Mtu mume akimwona kijana aliye mwanamwali ambaye hajaposwa, akamshika na kulala naye, wakaonekana;

29yule mtu mume aliyelala naye na ampe baba yake yule kijana shekeli hamsini za fedha, kisha na awe mkewe, kwa kuwa amemtweza; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote.

30Mtu mume asimtwae mke wa baba yake, wala asifunue ncha ya mavazi ya baba yake.