Kumbukumbu la Torati - Sura ya 26

1Na itakuwa, ukiisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi, na kuimiliki, na kukaa ndani yake;
2twaa malimbuko ya ardhi, utakayoyavuna katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako; ukayatie katika kikapu, ukaende hata mahali pale atakapopachagua Bwana, Mungu wako, ili alikalishe jina lake huko.
3Ukamwendee kuhani atakayekuwapo siku zile, ukamwambie, Ninakiri leo kwa Bwana, Mungu wako, ya kuwa nimeingia katika nchi Bwana aliyowaapia baba zetu ya kwamba atatupa.
4Naye kuhani atakipokea kikapu mkononi mwako, akiweke chini mbele ya madhabahu ya Bwana, Mungu wako.
5Nawe ujibu, ukaseme mbele za Bwana, Mungu wako, Baba yangu alikuwa Mwarami karibu na kupotea, akashuka Misri, akakaa huko ugenini, nao ni wachache hesabu yao; akawa taifa kubwa huko, yenye nguvu na watu wengi.
6Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito.
7Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu; Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu.
8Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu;
9naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali.
10Na sasa, tazama, nimeleta malimbuko ya mazao ya ardhi uliyonipa, Ee Bwana. Kisha ukiweke chini mbele za Bwana, Mungu wako, ukasujudu mbele za Bwana, Mungu wako;
11ukayafurahie mema yote ambayo Bwana, Mungu wako, amekupa, na nyumba yako, wewe, na Mlawi, na mgeni aliye kati yako.
12Utakapokwisha kutoa zaka, katika zaka zote za maongeo yako mwaka wa tatu, ambao ndio mwaka wa kutolea zaka, umpe zile zaka Mlawi, na mgeni, na yatima, na mjane, wapate kula ndani ya malango yako na kushiba;
13nawe sema mbele ya Bwana, Mungu wako, Vitu vilivyo vitakatifu nimeviondoa katika nyumba yangu, nami mimewapa Mlawi, na mgeni, na yatima, na mjane, kwa mfano wa maagizo yako uliyoniusia yote; sikukosa maagizo yako yo yote, wala sikuyasahau;
14katika vitu hivyo sikula wakati wa kukaa matanga mimi, wala sikuviondoa nikiwa na unajisi, wala sikutoa kwa ajili ya wafu katika vitu hivyo; sauti ya Bwana, Mungu wangu, nimeisikiza, nimefanya yote, kama ulivyoniamuru.
15Uangalie kutoka makazi yako matakatifu mbinguni, uwabarikie watu wako Israeli, na nchi uliyotupa kama ulivyowaapia baba zetu, nchi imiminikayo maziwa na asali.
16Leo hivi akuamuru Bwana, Mungu wako, kuzifanya amri hizi na hukumu; basi uzishike na kuzifanya kwa moyo wako wote na roho yako yote.
17Umemwungama Bwana leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake;
18naye Bwana amekuungama hivi leo kuwa taifa iliyotengwa iwe yake yeye, kama alivyokuahidi, na kuwa yakupasa kushika maagizo yake yote;
19na kuwa atakutukuza juu ya mataifa yote aliyoyafanya, kwa sifa, na jina, na heshima, nawe upate kuwa taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako, kama alivyosema.