Kumbukumbu la Torati - Sura ya 27

Kumbukumbu la Torati - Sura ya 27

1Musa na wazee wa Israeli wakawaagiza wale watu wakawaambia, Shikeni maagizo yote niwaagizayo leo.

2Na iwe, siku mtakayovuka Yordani kwenda nchi akupayo Bwana, Mungu wako, ujisimamishie mawe makubwa, ukayatalize matalizo,

3uyaandike maneno yote ya torati hii juu yake, utakapokwisha kuvuka; ili upate kuingia nchi akupayo Bwana, Mungu wako, nchi imiminikayo maziwa na asali, kama alivyokuahidi Bwana, Mungu wa baba zako.

4Na iwe, mtakapokwisha vuka Yordani myasimamishe mawe haya, niwaagizayo hivi leo, katika mlima Ebali, nawe yatalize matalizo.

5Na huko umjengee madhabahu Bwana, Mungu wako, madhabahu ya mawe, usitumie chombo cha chuma juu yake.

6Jenga hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wako, kwa mawe yasiyochongwa; ukamtolee Bwana, Mungu wako, sadaka za kuteketezwa juu yake;

7ufanye na sadaka za amani, ukale huko; nawe furahi mbele za Bwana, Mungu wako.

8Kisha, andika juu ya mawe hayo maneno ya torati hii yote, waziwazi sana.

9Musa na makuhani Walawi wakawaambia Israeli wote wakasema, Nyamaza, usikize, Ee Israeli; leo umekuwa watu wa Bwana, Mungu wako.

10Basi isikize sauti ya Bwana, Mungu wako, ufanye maagizo yake na amri zake nikuagizavyo leo.

11Musa akawaagiza wale watu siku iyo hiyo, akasema,

12Hawa na wasimame juu ya mlima wa Gerizimu kwa kuwabarikia watu, mkiisha vuka Yordani; Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Yusufu, na Benyamini;

13na hawa na wasimame juu ya mlima wa Ebali kwa laana; Reubeni, na Gadi, na Asheri, na Zabuloni, na Dani, na Naftali.

14Kisha Walawi na wajibu, wawaambie watu wote wa Israeli kwa sauti kuu,

15Na alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga, au ya kusubu, machukizo kwa Bwana, kazi ya mikono ya fundi, akaisimamisha kwa siri. Na watu wote wajibu, waseme, Amina.

16Na alaaniwe amdharauye baba yake au mama yake. Na watu wote waseme, Amina.

17Na alaaniwe aondoaye mpaka wa jirani yake. Na watu wote waseme, Amina.

18Na alaaniwe ampotezaye kipofu akakosa njia. Na watu wote waseme, Amina.

19Na alaaniwe apotoaye hukumu ya mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe. Na watu wote waseme, Amina.

20Na alaaniwe alalaye na mke wa baba yake, kwa kuwa amefunua mavazi ya babaye. Na watu wote waseme, Amina.

21Na alaaniwe alalaye na mnyama wa aina yo yote. Na watu wote waseme, Amina.

22Na alaaniwe alalaye na umbu lake, binti ya babaye, au binti ya mamaye. Na watu wote waseme, Amina.

23Na alaaniwe alalaye na mkwewe, mamaye mkewe. Na watu wote waseme, Amina.

24Na alaaniwe ampigaye mwenzake kwa siri. Na watu wote waseme Amina.

25Na alaaniwe atwaaye ujira wa kumwua asiye makosa. Na watu wote waseme, Amina.

26Na alaaniwe asiyeyaweka imara maneno ya torati hii kwa kuyafanya. Na watu wote waseme, Amina.