Kumbukumbu la Torati - Sura ya 30

1Tena itakuwa, mambo haya yote yatakapokujilia, baraka na laana nilizoweka mbele yako, nawe utakapozikumbuka kati ya mataifa yote, huko atakakokupeleka Bwana, Mungu wako,
2nawe utakapomrudia Bwana, Mungu wako, na kuitii sauti yake, mfano wa yote nikuagizayo leo, wewe na wanao, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote;
3ndipo Bwana, Mungu wako, atakapougeuza utumwa wako, naye atakuhurumia, tena atarejea na kukukusanya kutoka mataifa yote, huko alikokutawanyia Bwana, Mungu wako.
4Watu wako waliotawanyika wakiwako katika ncha za mbingu za mwisho, kutoka huko atakukusanya Bwana, Mungu wako; kutoka huko atakutwaa;
5atakuleta Bwana, Mungu wako, uingie nchi waliyomiliki baba zako, nawe utaimiliki; naye atakutendea mema, na kukufanya uwe watu wengi kuliko baba zako.
6Bwana, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai.
7Na laana hizi zote Bwana, Mungu wako, atawatia adui zako na hao wakuchukiao, waliokuwa wakikutesa.
8Nawe utarudi, uitii sauti ya Bwana, na kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo.
9Na Bwana, Mungu wako, atakufanya uwe na wingi wa uheri katika kazi yote ya mkono wako, katika uzao wa tumbo lako, na katika uzao wa ng'ombe wako, na katika uzao wa nchi yako; kwa kuwa Bwana atafurahi tena juu yako kwa wema, kama alivyofurahi juu ya baba zako;
10ukiwa utaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote.
11Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali.
12Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?
13Wala si ng'ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?
14Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.
15Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya;
16kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki.
17Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia;
18nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia; hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki.
19Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako;
20kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.