Kumbukumbu la Torati - Sura ya 5
1Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na hukumu ninenazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuangalia kuzitenda.
2Bwana, Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu.
3Bwana hakufanya agano hili na baba zetu, bali na sisi, yaani, sisi sote tuliopo hapa, tu hai.
4Bwana alisema nanyi uso kwa uso mlimani, toka kati ya moto;
5(nami wakati ule nalisimama kati ya Bwana na ninyi, ili kuwaonyesha neno la Bwana; maana, mliogopa kwa sababu ya ule moto, wala hamkupanda mlimani); naye akasema,
6Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.
7Usiwe na miungu mingine ila mimi.
8Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi.
9Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,
10nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.
11Usilitaje bure Jina la Bwana, Mungu wako; maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia, mtu alitajaye jina lake bure.
12Ishike siku ya Sabato uitakase, kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru.
13Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote;
14lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako ye yote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe.
15Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa Bwana, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato.
16Waheshimu baba yako na mama yako; kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.
17Usiue.
18Wala usizini.
19Wala usiibe.
20Wala usimshuhudie jirani yako uongo.
21Wala usimtamani mke wa jirani yako; wala usiitamani nyumba ya jirani yako, wala shamba lake, wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala kitu cho chote alicho nacho jirani yako.
22Haya ndiyo maneno ambayo Bwana aliwaambia mkutano wenu wote mlimani kwa sauti kuu toka kati ya moto, na wingu, na giza kuu; wala hakuongeza neno. Akayaandika juu ya mbao mbili za mawe, akanipa.
23Ikawa, mlipoisikia sauti ile toka kati ya giza, na wakati uo huo mlima ule ulikuwa ukiwaka moto, basi, mlinikaribia, naam, wakuu wote wa kabila zenu, na wazee wenu,
24mkasema, Tazama, Bwana, Mungu wetu, ametuonyesha utukufu wake, na ukuu wake, nasi tunasikia sauti yake toka kati ya moto; mmeona leo ya kuwa Mungu husema na mwanadamu, naye akaishi.
25Sasa basi, mbona tufe? Maana moto huu mkubwa utatuteketeza; tukiisikia tena sauti ya Bwana, Mungu wetu, tutakufa.
26Maana katika wote wenye mwili ni nani aliyeisikia sauti ya Mungu aliye hai, akisema toka kati ya moto, kama vile sisi, asife?
27Enenda karibu wewe, ukasikie yote atakayoyasema Bwana, Mungu wetu; ukatuambie yote atakayokuambia Bwana, Mungu wetu; nasi tutayasikia na kuyatenda.
28Naye Bwana akasikia sauti ya maneno yenu mliyoniambia; Bwana akaniambia, Nimesikia sauti ya maneno ya watu hawa waliyokuambia; wamesema vema yote waliyosema.
29Laiti wangekuwa na moyo kama huu ndani yao sikuzote, wa kunicha, na kushika amri zangu zote sikuzote, wapate kufanikiwa wao na watoto wao milele!
30Enda uwaambie, Rudini hemani mwenu.
31Lakini wewe, simama hapa karibu nami, nami nitanena nawe sheria zote, na amri na hukumu, utakazowafunza, wapate kuzifanya katika nchi niwapayo kuimiliki.
32Tunzeni basi, mtende kama mlivyoamriwa na Bwana, Mungu wenu; msikengeuke kwa mkono wa kuume wala wa kushoto.
33Endeni njia yote aliyowaagiza Bwana, Mungu wenu, mpate kuwa hai, na kufanikiwa, mkafanye siku zenu kuwa nyingi katika nchi mtakayoimiliki.

Swahili
Italiano (it-IT)
Português do Brasil (pt-BR)
Polski (PL)
Deutsch (Deutschland)
Français (France)
Español (España)
Українська Біблія у перекладі Огієнка
English Bible - 21ST CENTURY KING JAMES (KJ21)