Kumbukumbu la Torati - Sura ya 9

Kumbukumbu la Torati - Sura ya 9

1Sikiza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita wewe, miji mikubwa iliyojengewa kuta hata mbinguni,

2watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki?

3Basi jua siku hii ya leo kuwa Bwana, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia Bwana.

4Usiseme moyoni mwako, Bwana, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia Bwana niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya Bwana awafukuza nje mbele yako.

5Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya Bwana, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno Bwana alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.

6Basi jua ya kuwa Bwana, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu.

7Kumbuka, usisahau ulivyomtia Bwana, Mungu wako, kasirani jangwani; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hata mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya Bwana

8Tena mlimkasirisha Bwana katika Horebu, Bwana akakasirika nanyi hata akataka kuwaangamiza.

9Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano Bwana alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji.

10Bwana akanipa zile mbao mbili za mawe zimeandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote aliyosema nanyi Bwana mle mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano.

11Ikawa mwisho wa siku arobaini usiku na mchana, Bwana alinipa zile mbao mbili za mawe, nazo ni mbao za agano.

12Bwana akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu.

13Tena Bwana akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu;

14niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao.

15Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili.

16Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya Bwana, Mungu wenu; mmefanya ndama ya ng'ombe ya kusubu; mmekengeuka upesi katika njia aliyowaamuru Bwana.

17Nikazishika zile mbao mbili, nikazitupa kutoka katika mikono yangu miwili, nikazivunja mbele ya macho yenu.

18Nikaanguka nchi mbele za Bwana siku arobaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyokosa, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, kwa kumkasirisha.

19Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia Bwana kutaka kuwaangamiza. Lakini Bwana alinisikiza wakati huo nao.

20Bwana akamkasirikia sana Haruni akataka kumwangamiza; nikamwombea Haruni naye wakati huo.

21Kisha nikaitwaa ile dhambi yenu, huyo ndama mliyemfanya, nikamteketeza kwa moto, nikamponda, nikamsaga tikitiki, hata akawa laini kama vumbi; nikalitupa vumbi lake katika kijito kilichoshuka kutoka mlimani.

22Tena huko Tabera, na Masa, na Kibroth-hataava mlimtia Bwana hasira.

23Na wakati alipowatuma Bwana kutoka Kadesh-barnea, akiwaambia, Kweeni mkaimiliki nchi niliyowapa; ndipo mkaasi juu ya maagizo ya Bwana, Mungu wenu, hamkumsadiki wala hamkusikiza sauti yake.

24Mmekuwa na uasi juu ya Bwana tokea siku nilipowajua ninyi.

25Ndipo nikaanguka nchi mbele za Bwana siku zile arobaini usiku na mchana nilizokuwa nimeanguka nchi; kwa kuwa Bwana alisema atawaangamiza.

26Nikamwomba Bwana, nikasema, Ee Bwana Mungu, usiwaangamize watu wako, urithi wako, uliowakomboa kwa ukuu wako, uliowatoa Misri kwa mkono wa nguvu.

27Wakumbuke watumwa wako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; usiangalie upotofu wa watu hawa, wala uovu wao, wala dhambi yao;

28isije nchi uliyotutoa ikasema, Ni kwa sababu Bwana hakuweza kuwaleta katika nchi aliyowapa ahadi, tena ni kwa kuwa aliwachukia, alivyowatoa nje ili kuwaua jangwani.

29Nao ni watu wako, urithi wako, uliowatoa kwa nguvu zako kuu na mkono wako ulionyoka.